"Huyo jamaa sio msanii!" Khaligraph apuuzilia mbali madai ya Erick Omondi kwamba sekta ya muziki nchini imekufa

Rapa huyo alisema nchi ya Kenya inafanya vizuri sana kimuziki.

Muhtasari

•Khaligraph alisema kunao wasani wengi nchini ambao  wangali wanatia bidii kwenye muziki kuhakikisha kwamba sekta hiyo imeendelea kukua.

•Khaligraph aliwasihi Wakenya kuacha kulinganisha sekta ya burudani nchini na mataifa mengine kama Tanzania na Afrika Kusini huku akidai kuwa kimuziki Kenya inashindwa tu na Nigeria 

Khaligraph na Erick Omondi
Khaligraph na Erick Omondi
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za kufoka Brian Ouko almaarufu kama Khaligraph Jones amepuuzilia mbali madai ya mchekeshaji Eric Omondi kwamba sekta ya burudani nchini imekufa kwani wasanii wamelala.

Alipokuwa anahutubia waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa chapa ya Galactic siku ya Jumamosi, rapa huyo  alisema nchi ya Kenya inafanya vizuri sana kimuziki.

Khaligraph aliwasihi Wakenya kuacha kulinganisha sekta ya burudani nchini na mataifa mengine kama Tanzania na Afrika Kusini huku akidai kuwa kimuziki Kenya inashindwa tu na Nigeria .

"Kenya inafanya vizuri sana kimuziki. Hata Tanzania haitushindi. Diamond siye msanii pekee Tanzania eti kila wakati  anatumika kulinganisha na wasanii wa Kenya. Sisi tuko mahali sawa na tunafanya vizuri. Watu wakianza kusema eti Kenya iko nyuma wanafaa kuangalia kuna mataifa mangapi Afika. Tuko na mataifa 54. Bila kuhesabu Nigeria, hakuna nchi nyingine inashinda Kenya kimuziki. Nigeria iko na watu milioni 200. Afrika Kusini hawawezi tupiku" Khaligraph alisema.

Khaligraph alisema kunao wasani wengi nchini ambao  wangali wanatia bidii kwenye muziki kuhakikisha kwamba sekta hiyo imeendelea kukua.

Rapa huyo ametoa ombi kwa Wakenya waache kufuatilia madai ya Eric Omondi huku akieleza kuwa yeye sio mwanamuziki bali ni mchekeshaji.

"Huyo jamaa sio msanii. Eric Omondi anafaa kuhutubia wachekeshaji!" Alisema.

Alisema hana shida yoyote na katungulia kwenye jukwaa kabla ya mwanamuziki mwingine wakati wa tamasha.

Siku kadhaa zilizopita Eric Omondi aliwasihi wasanii wa Kenya waamke huku akidai kuwa wengi wao wameisha, wamezembea  na wanachosha.

"Tumekuwa wa kutohitajika, wa kutabirika na wa kuchosha. Tunahitaji kutia bidiii zaidi ili turudishe utukufu uliopotea. Lazima tuwekeze kwa sanaa. Mungu anajua mimi najaribu kadri  niwezavyo" Omondi amesema.

Omondi alidai kuwa bendi ya Sauti Sol, rapa Khalighraph Jones na mwanamuziki aliyegura injili Bahati pekee ndio tumaini ya sekta ya burudani nchini.

Hata hivyo amesema kwamba ubabe wao katika sanaa umekuwa ukididimia tangu walipopiga hatua ya kufunga ndoa.

"Hatua ya kwanza ya kutatua tatizo lolote ni kukubali kwamba tasnia yetu ya muziki haijawa sawa. Ujumbe wangu ni kuwa tulipoteza kitu na wazo langu ni pamoja tunaweza kuitafuta na kuirudisha. @sautisol @khaligraph_jones na  @bahatikenya nyinyi ndio tumaini letu lakini ukweli usemwe, tangu muoe mambo hayajakaa sawa😥😥😥. Siwezi kukaa na kutazama sekta yetu ya muziki ikilala na kunyamaza kabisa, Lazima tu nifungue roho. @sautisol najua tuko peke pamoja na tunashukuru kila wimbo mmetoa kibinafsi lakini kikundi kikinyamaza ni sekta na mashabiki ndio wanaumia. Hata sijui kwanini nawabembeleza. AMKENI BWANAAA!!! AMKENIIIII MUMELALAAA na huo ndio UKWELI MKUBWA!!!! @bienaimesol wewe Nunua WIG kwanza ufunike KIPARA kabla ya uongeleshe  rais. Shenzi" Omondi amesema.

Wanamitandao wengi ikiwemo wasanii kadhaa kama Jua Cali, Khaligraph, Bien, Femi One na Svara wamejitokeza kukosoa maneno ya Omondi.