Size 8 azungumzia afya yake baada ya kulazwa hospitalini kutokana na shinikizo la damu

Muhtasari

•Size 8 amewashukuru wote ambao walimuombea na madaktari waliomhudumia huku akisema anatumai kupewa ruhusa kutoka hospitalini hivi karibuni

•Mwanamuziki huyo alilazwa hospitalini siku ya Alhamisi baada ya kukumbwa na shinikizo la damu.

Image: INSTAGRAM// SIZE 8 REBORN

Mwimbaji wa nyimbo za injili Linet Munyali almaarufu Size 8 amefichua kuwa anaendelea kupata afueni baada ya kulazwa hospitalini siku chache.

Katika taarifa ambayo alitoa Jumamosi, Size 8 alisema kwa sasa anahisi nafuu na hayuko tena hatarini.

Mama huyo wa watoto wawili aliwashukuru wote ambao walimuombea na madaktari waliomhudumia huku akisema anatumai kupewa ruhusa kutoka hospitalini hivi karibuni.

"Wakati hatuelewi kwa nini baadhi ya mambo hutokea inatubidi tu kuwa na matumaini na kutegemea upendo wa milele usio na mwisho wa Mungu. Nimetoka hatarini sasa ninajisikia vizuri zaidi na ninaamini kwamba yote yatakuwa vizuri. Asanteni sana wote mlioniombea, Mungu awabariki, Maombi yenu yote Bwana ameyasikia... Madaktari kwa mara nyingine tena Mungu awabariki sana kwa kinishughulikia bila kuchoka. Natumai kupewa ruhusa hivi karibuni," Size 8 alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mwanamuziki huyo alilazwa hospitalini siku ya Alhamisi baada ya kukumbwa na shinikizo la damu.

Kanda ya video ambayoilipakiwa Instagram  ilionyesha akiwa mdhaifu huku wahudumu wawili wa afya wakijitahidi kumzuia asianguke.

DJ Moh akizungumza na Mpasho alifichua kuwa mkewe alilazwa baada ya kukumbwa na shinikizo la damu.

"Alikimbizwa hospitali na kulazwa kutokana na shinikizo la damu, anaendelea vizuri zaidi sasa," DJ Moh alisema.

Mwaka jana mama huyo wa watoto wawili alipoteza ujauzito kutokana na tatizo hilo la shinikizo la damu.