Rayvanny anadaiwa Tsh1B kukatisha mkataba na Wasafi? - Diamond aweka mambo wazi

Muhtasari

•Diamond alisema kuwa Rayvanny ana nidhamu kubwa na hawezi kuondoka pale kwa njia isiyo ya heshima.

Diamond Platnumz na Rayvanny
Diamond Platnumz na Rayvanny
Image: HISANI

Bosi wa Wasafi Diamond Platnumz amefutilia mbali tetesi kuwa msanii wake Rayvanny anakusudia kuigura lebo hiyo.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Diamond alisema kuwa Rayvanny ana nidhamu kubwa na hawezi kuondoka pale kwa njia isiyo ya heshima.

Diamond alikanusha madai kuwa anamdai msanii huyo ambaye alijiunga na Wasafi mwaka wa 2015 shilingi bilioni moja za Tanzania ili kumruhusu akatishe mkataba wake na lebo hiyo yake.

"Hamna kitu kama hicho. Ikifikia anataka kuondoka haiwezi kutokea tatizo. Rayvanny najua sio mjinga wa kuambiwa maneno. Katika Wasafi tuna lengo kuwa lazima msanii akue. Tunajua lazima msanii akue. Rayvanny ana nidhamu sana. Kwa ukubwa aliofikia Rayvanny angekua mwehu tangu kitambo, angewez kunivunjia heshima kitambo. Angekuwa mwehu mwingine pengine anataka kuanzisha lebo, angetumia akili aongee na timu wakakubaliana na kuanzisha lebo. Ikitokea siku Rayvanny anataka kuondoka Wasafi, siamini anaweza kuondoka kiwendawazimu ,"  Diamond alisema.

Diamond aliweka wazi kuwa kukosekana kwa Rayvanny katika hafla za Wasafi za hivi karibuni hakumaanishi kuwa anakusudia kuondoka bali ni kwa sababu amekuwa bize na kazi zingine muhimu.

Hali kadhalika alisema kuwa dili zingine za nje ambazo Rayvanny amekuwa akichukua ni kwa manufaa ya WCB.

"Ukiona sijafanya kitu kikubwa, utaona Rayvanny kafanya.  Sisi tunatafuta matokeo ya kidunia maana ya Afrika tushafanya. Tunataka tuende mbali zaidi... Lengo letu ni kupiga hela mpaka watu wachanganyikiwe," Diamond alisema.

Katika kipindi cha miezi ya hivi majuzi kumekuwa na tetesi kwamba Rayvanny anapanga kuondoka Wasafi na kuanzisha lebo yake. Mwaka uliopita Harmonize aliibua madai kuwa Rayvanny alimfichulia kuwa haridhiki na lebo hiyo.