Muigizaji Kevin Mwangi 'Shaniqwa' asimulia alivyojipata akiigiza kama mwanamke kinyume na matarajio yake

Muhtasari

•Mwangi alisema kuwa alipatiwa nafasi ile na mwelekezaji wa filamu baada ya mwanadada aliyekuwa amepangwa kuwa mhusika katika shoo fulani aliyokuwa ameenda kushuhudiwa ikirekodiwa kukosa kufika.

•Baada ya kukubali kuchukua nafasi ile Mwangi alienda kwa kinyozi na kunyolewa ndevu zote  kisha akapondolewa uso mara moja.

• Hata hivyo alijipata katika hali ya mtanziko kwa kuwa mapenzi yake hayakuwa kuigiza kama mwanamke. 

Mwigizaji Kelvin Mwangi almaarufu kama Shaniqwa
Mwigizaji Kelvin Mwangi almaarufu kama Shaniqwa
Image: HISANI

Mwigizaji na mcheshi mashuhuri Kevin Mwangi amefichua alivyoanza kuigiza kama mwanadada aliyejitambulisha kama 'S

Akiwa kwenye mahojiano na Jeff Kuria, mzaliwa huyo wa kaunti ya Kirinyaga alieleza kuwa alipata jukumu hilo baada ya majaribio mengi ya kuigiza kama rais Uhuru Kenyatta kugonga mwamba.

Mwangi alisema kuwa alipatiwa nafasi ile na mwelekezaji wa filamu baada ya mwanadada aliyekuwa amepangwa kuwa mhusika katika shoo fulani aliyokuwa ameenda kushuhudiwa ikirekodiwa kukosa kufika.

"Mwelekezaji filamu alikuwa na kipengele ambapo alitaka 'slay queen' na mpenzi wake ambao walikuwa wanakosania kwa hoteli ju ya chakula na mambo mengine. Nilienda pale nikaketi. Msichana ambaye alikuwa anatarajiwa kucheza sehemu ile hakufika. Mwelekezaji filamu alianza kuulizia mahali mwanadada huyo alikuwa amefika, mwishowe akasema kuwa hangeweza kufika" Mwangi alisimulia.

Baada ya mhusika huyo kukosa kufika mwelekezaji filamu alianza juhudi za kutafuta mwanamke mwingine ambaye angejaza pengo lile ila hakuna aliyekuwa anapatikana karibu. Kwa kuwa lazima filamu ingeendelea kutengenezwa aliamua kutafuta mwanaume ambaye angeweza kuigiza kama mwanamke.

Mwangi alieleza kuwa mwelekezaji filamu alimchagua kwa kuwa hapo awali aliwahi kuwa mhusika kwa shoo nyingine ambayo wanaume waliigiza kama wanaume.

 Hata hivyo alijipata katika hali ya mtanziko kwa kuwa mapenzi yake hayakuwa kuigiza kama mwanamke. Alikiri kwamba haukuwa mpango wake kuigiza kama mwanamke.

"Mwelekezaji alininyooshea kidole akaniambia kwa kuwa nilikuwa Comedy Club na kwa wakati mwingine tulikuwa tunaigiza kama wanawake nichukue nafasi hiyo. Aliahidi kunipatia kandarasi. Lakini nilitaka kuwa 'cool celeb' kama Nick Mutuma. Nilitaka wasichana wawe wakinikufia kila waliponiona. Nilichanganyikiwa kama ningechukua kandarasi ile ama niache. Nilipokumbuka mashida zangu nikamwambia ni sawa" Alisema Mwangi.

Baada ya kukubali kuchukua nafasi ile Mwangi alienda kwa kinyozi na kunyolewa ndevu zote  kisha akapondolewa uso mara moja.

Mwigizaji huyo alieleza kwamba alicheza vizuri mno hadi akafurahisha watengeneza filamu na waigizaji waliokuwa pale.

Hata hivyo hakujua papo hapo iwapo alikuwa amefuzu kuigiza nafasi ile na alikuja kugundua baadae baada ya marafiki wake kumwambia kuwa walimuona kwa runinga.

"Siku moja nikiwa natembea Kayole nilipatana na rafiki yangu akaniambia kuwa aliniona kwa runinga, nikashindwa aliniona wapi kwa runinga nikamwambia alikuwa amekosea sura. Tukapatana na mwingine akaniambia vilevile. Nikapigia wale watu walikuwa wanatengeneza shoo hiyo, Terence Creative alikuwa mwelekezaji pale. Aliniambia kuwa nilikuwa nimechukuliwa.  Nilihisi vizuri. Akaniambia nipigie mzalisha filamu. Mzalisha filamu akaniambia kuwa walikuwa wamenitafuta kwa sana" Alisema.

Baada ya mazungumzo hayo alienda hadi ofisini mkubwa wa Televisheni na akapewa kandarasi ya kuigiza kama 'Shaniqwa'