"Nilikuwa nakufa, nilikuwa nadungwa mfupa nikitazama" King Kaka asimulia mambo ya kutisha yaliyomkumba hospitalini

Muhtasari

•Rapa huyo alifichua alipitia wakati mgumu sana alipokuwa amelazwa hospitali huku akisema alipambana sana kujitoa pale

•Alisema aliwapeza watoto wake sana alipokuwa kitandani cha hospitali ila hakutaka kuwaambia kuhusu ugonjwa wake.

•Alitaja baadhi ya masaibu na machungu ambayo yalimkumba ikiwemo kutapika na kudamu na kukosa nguvu ya kutembea.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka alizindua EP yake 'Happy Hour' usiku wa Jumanne.

Kaka alitumia fursa ile kuzungumza kuhusu afya yake kwa sasa na hali ilivyokuwa wakati alikuwa amelazwa hospitali miezi michache iliyopita.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, King Kaka alisema sasa  anajihisi kama mtoto mchanga kwani kulingana naye anaishi maisha yake ya pili.

Rapa huyo alifichua alipitia wakati mgumu sana alipokuwa amelazwa hospitali huku akisema alipambana sana kujitoa pale.

"Nilipoteza matumaini, nilipigana tena na tana. Palikuwa pahali pa kusikitisha sana na penye giza" Alisema King Kaka.

King Kaka alisema watoto wake ndio walimpatia sababu za kuendelea kupambana na ugonjwa uliokuwa umemuathiri kwa zaidi ya miezi mitatu.

Alisema aliwapeza watoto wake sana alipokuwa kitandani cha hospitali ila hakutaka kuwaambia kuhusu ugonjwa wake.

"Walinipatia sababu za kupambana. Nilikuwa nawamiss sana. Nilikuwa nimewaficha, sikutaka kuwaambia eti mi ni mgonjwa. Wakati mwingine ningewapigia simu na wangenifanya nicheke. Lakini nilikuwa naona hapa naenda" Alisema.

Mwanamuziki huyo alitaja baadhi ya masaibu na machungu ambayo yalimkumba ikiwemo kutapika na kudamu na kukosa nguvu ya kutembea.

"Nilikuwa nakufa, nilikuwa natapika na kukojoa damu. Nilikuwa nadungwa mifupa nikiona. Walikuwa wanatoa dondoo pale. Saa hii nakula, natembea. Ni maisha yangu ya pili" Kaka alisema.

King Kaka alisema alikosa kujulisha watu kuhusu masaibu aliyokuwa anapitia kwa sababu huwa anapendelea kupigana vita vyake kivyake. 

"Niliambia mashabiki wangu waniombee tu. Sikutaka pesa wala kitu chochote" Alisema.