"Najuta siku niliyopata umaarufu!" Akothee alalamika

Muhtasari

•Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 amewasihi mashabiki wake kusita kuchukua picha asizotarajia huku akiwaarifu kwamba hayuko sawa kabisa kwa sasa.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu kama Akothee haridhishwi na uangalizi ambao kwa kawaida huwa anapewa kila anapokuwa hadharani kutokana na hali yake ya kuwa mtu mashuhuri.

Akothee ametumia ukurasa wake wa Instagram kulalamika kuhusu jinsi watu wanavyosisitiza kupiga naye picha kila mara bila kujali hali yake ya afya na anachopitia kwa wakati huo.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 amewasihi mashabiki wake kusita kuchukua picha asizotarajia huku akiwaarifu kwamba hayuko sawa kabisa kwa sasa.

" Najuta siku nilipata umaarufu, huu upuuzi haufurahishi. Hata nikiwa na kifaa cha kushikilia shingo na sura ya kuchekesha, watu wengine bado wanasisitiza kuchukua  selfie . Eeee Hivi kweli ni mapenzi ama ni kitu sijui ? Wakati mwingine mimi naumia na najaribu kusukuma kidogo tu maisha! Niepushe na picha za nisizotarajia TafadhaliI! Najua mnapenda ushahidi! Ngonjeni kidogo. Mwaka huu ulianza na kipindi kibaya kwangu! Hata nguvu ya kupiga picha Sina!! mtanisamehe" Akothee amesema.

Mama huyo wa watoto watano ameelezwa kwamba kunazo nyakati huwa anaenda dukani na mashabiki wengine wanatoa simu zao na kuanza kumrekodi bila yeye kujua na hata bila kumsalimia kwanza.

Amefichua kwamba kuna wakati nusura alimane mangumi na mateke na mmoja wa mashabiki kama wale ambaye alimuongelesha shemeji wake vibaya alipomnasa akiwarekodi.

"Ukiwaona wanajificha. Nilikaribia kupigana na mmoja ambaye alikua mkorofi sana kwa shemeji yangu ambaye alimshika na movie nzima ya mimi na familia yangu tukifanya shopping. Nini kinaendelea?" Akothee amelalamika.

Akothee anatambulika sana kutokana na muziki wake na utata mwingi uliozingira maisha yake. Huwa amejibandika jina 'rais wa single mothers' kutokana na hali yake ya kulea watoto watano bila usaidizi wa mwanamume.