'Nilikuwa nalala juu ya pesa,' Magix Enga afichua aliyopitia Illuminati na anavyoandamwa baada ya kugura

Muhtasari

•Msanii huyo amesema alianza kupokea mamilioni ya pesa baada ya kukubali wito wa kujiunga na madhebehu hayo.

•Amesema alifikia maamuzi ya kugura baada ya kuanza kupatiwa maagizo ambayo hangeweza kutimiza.

Image: MAGIX ENGA

Mwanamuziki na mzalishaji tajika nchini Magix Enga amefunguka kuhusu yale aliyopitia baada ya kujiunga na Illuminati.

Akiwa kwenye mahojiano na Plug TV, Magix alikiri kwamba umaskini ulimshinikiza kukubali kujiunga na madhebehu hayo baada ya mwanadada mmoja kujitolea kumsaidia kujipatia utajiri mkubwa kutokana na  taaluma yake.

Msanii huyo amesema alianza kupokea mamilioni ya pesa baada ya kukubali wito wa kujiunga na madhebehu hayo.

"Kila mwezi nilikuwa napokea pesa. Kuna gari fulani ilikuwa inakuja kila mwezi naambiwa niingie. Nilikuwa nakalia kiti cha nyuma lakini sikuwa naangalia ni nani alikuwa anaendesha. Ningechukua pesa zangu kisha narudi studioni. Nilikuwa napata pesa  nyingi. Mfuko huo haukuwa unakosa  kitu kama milioni tano, wakati mwingine nilipata milioni saba. Ilikuwa pesa nyingi, nilikuwa nalala juu ya pesa" Magix Enga alisema.

Mzalishaji huyo aliweka wazi kwamba hakuna karatasi zozote ambazo alitia saini na hakuna mtu yeyote ambaye alitoa kafara ila wangechukua damu yake mara kwa mara.

"Huwa wanachukua damu pekee yake. Walikuwa wananipigia simu wananiambie niende nje ya lango nichukue mfuko wangu. Walinitoa damu kwa tumbo" Alisema.

Magix alisema licha ya manufaa yote ya kifedha ambayo alikuwa anapata ilifikia hatua akasema imetosha na kuamua kuondoka.

Amesema alifikia maamuzi ya kugura baada ya kuanza kupatiwa maagizo ambayo hangeweza kutimiza.

"Ilifika hatua fulani wakawa wanadai vitu zingine ambazo singeweza kuwapatia. Siwezi zisema ili nisishtue watu, hiyo ni dunia nyingine. Nilijificha miaka miwili. Nilijawa na hofu kiasi cha kwamba niliwaza kujitoa uhai" Magix alisema.

Msanii huyo aliweka wazi kwamba kwa sasa hayuko tena katika kikundi hicho na tayari amemkubali yesu na kuokoka. 

Hata hivyo amefichua kwamba bado anaendelea kuwindwa na wanachama wa madhebehu hayo.

"Nafuatwa kila mahali. Ndio maana siwezi toa barakoa. Siwezi waongelea bila barakoa. Mimi nimeokoka sana sasa. Hata napanga kufungua kanisa li nizidi kusaidia wasee wanapitia  mambo kama  ile napitia na kuwaonyesha mwelekeo wa kuwa waumini. Ata kama sitakuwa mhubiri, nitakuwa na kanisa" Alisema.

Hivi majuzi msanii huyo alifichua kwamba alijiunga na Illuminati akiwa na umri wa miaka 23 akikusudia  kuinua taaluma yake ya usanii.