Mchekeshaji Akuku Danger alazwa hospitalini tena kufuatia matatizo ya kupumua

Muhtasari

•Mwigizaji Sandra Dacha amefichua kwamba Akuku amelazwa katika chumba maalum cha wagonjwa cha HDU.

Mchekeshaji Akuku Danger alazwa tena siku chache tu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini
Mchekeshaji Akuku Danger alazwa tena siku chache tu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini
Image: INSTAGRAM// SANDRA DACHA

Siku chache tu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali, mchekeshaji wa Churchill Show Akuku Danger amelazwa tena.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwigizaji Sandra Dacha almaarufu kama Silprosa amefichua kwamba Akuku amelazwa katika chumba maalum cha wagonjwa cha HDU.

Dacha ameeleza kwamba mchekeshaji huyo alilazwa Jumapili baada ya kuathiriwa tena na matatizo ya kupumua.

"Tumerudi hospitalini tena. Matatizo ya kupumua tena. Yuko katika HDU tunapozungumza. Endeleeni kumwombea Akuku Danger" Dacha alitangaza.

Akuku Danger aliruhusiwa kwenda nyumbani wiki iliyopita baada ya kuwa amelazwa kwa kipindi cha wiki kadhaa.

Mchekeshaji huyo alilazwa katika hospitali ya Nairobi mwishoni mwa mwaka jana baada ya kushambuliwa na ugonjwa wa Pneumonia.

Dacha ambaye hivi majuzi aliweka wazi mahusiano kati yake na mchekeshaji huyo amewasihi Wakenya kuendelea kumwombea mpenzi wake apate afueni.

"Endelea kupambana mpenzi!" Dacha amemtia moyo Akuku Danger.

Mamia ya wanamitandao wameendelea kumtakia Akuku Danger afueni ya haraka.