Mcheshi Akuku Danger aruhusiwa kutoka hospitalini

Muhtasari

• Ni rasmi kwamba mcheshi Akuku Danger atakuwa anaruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kulazwa kwa muda mrefu sasa.

• Amewashukuru  mashabiki wote ambao wamesaidia pakubwa katika maombi, kuchanga hela na usaidizi wowote katika mchakato wa kuhakikisha anapata nafuu .

Akuku Danger
Akuku Danger
Image: INSTAGRAM

Ni rasmi kwamba mcheshi Akuku Danger atakuwa anaruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kulazwa kwa muda mrefu sasa.

Kupitia video aliyotupia katika mtandao wa Instagram, Akuku Danger amesema kwamba Mungu alimpa nafasi ya kupumzika na kujirudi kupitia ugonjwa wake ili ajipange kurejea kwenye jukwaa kwa njia bora zaidi. Ameendelea kuwashukuru mashabiki wote ambao wamesaidia pakubwa katika maombi, kuchanga hela na usaidizi wowote katika mchakato wa kuhakikisha anapata nafuu na kurejelea hali yake ya kawaida.

"Nasikia watu wakisema nilikuwa mgonjwa, hapana, Mungu alisema nipumzike kidogo. Majokes Nimeandika sahizi guys I can't wait to be back on stage maze, " alisema Akuku Danger.

Licha ya furaha machoni mwa mcheshi huyo na hata mashabiki wake, kuna hali ya atiati kwani bado kuna ada ya shilingi milioni mbili ambayo inapaswa kulipwa ili msanii huyo aruhusiwe kuondoka rasmi hospitalini, huku akiwaomba Wakenya kujisukuma zaidi katika kutoa mchango na kumsaidia kuondoka hospitalini humo ili kuendelea na mishe zake za kawaida.

Image: INSTAGRAM/ SANDRA DACHA

Mashabiki pia wameonekana kuvutiwa na ukarimu wa Sandra Dacha ambaye ni mchumba wake Akuku Danger, ambaye ameonekana kusimama na mpenzi wake katika kipindi hiki chote amekuwa akiugua. Dacha amechapisha bango kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwasihi mashabiki wasichoke kumsaidia mpenziye hadi pale atakapomaliza kugharamikia ada ya matibabu.

Katika kipindi cha hivi karibuni, wasanii wengi wameonekana kujikuta katika hali tata kihela huku mashabiki wakijikuna vichwa kuhusu ni vipi wasanii wa Kenya wanatumia senti wanazozitengeneza kupitia sanaa yao. Aidha mashabiki wameombwa kuwapa sapoti wasanii bila kukashifu na kukemea jinsi wasanii hawa wanavyofanikisha maisha Yao.

La mno kwa sasa ni kusubiri kuona wakenya watachangamka kiasi gani kuhakikisha mcheshi huyo mahiri ametoka hospitalini, na tunakuhakikishia kwamba tutakuletea habari hiyo pindi itakapochipuka.