Shaniqwa asimulia jinsi Itumbi alivyokatiza ndoto yake ya uigizaji katika shule ya upili

Muhtasari

•Mwangi alisema alianza kukuza kipawa chake cha uigizaji akiwa katika shule ya upili ya Nyang'wa iliyo katika kaunti ya Embu.

•Alifichua kwamba hakuwahi pita hatua ya Mkoa huku akimlaumu mwanablogu mashuhuri Denis Itumbi kwa masaibu yake.

Mwigizaji Kevin Mwangi na Shaniqwa
Mwigizaji Kevin Mwangi na Shaniqwa
Image: HISANI

Mwigizaji Kelvin Mwangi anayejulikana zaidi  kama Shaniqwa amesema kwamba alianza kuigiza  na umri mdogo akiwa bado anasoma katika shule ya upili.

Akiwa kwenye mahojiano na Ala C katika kipindi cha Reke Ciume na Ene, Mwangi alisema alianza kukuza kipawa chake cha uigizaji akiwa katika shule ya upili ya Nyang'wa iliyo katika kaunti ya Embu.

"Nilipojiunga na Nyang'wa Boys nilienda kujifunza uigizaji. Hata nilifufua klabu ya drama ya shule hiyo" Mwangi alisema.

Mwigizaji huyo alisema wakati alipokuwa anasoma alibobea sana katika uigizaji na kuwabwaga washindani kutoka shule zingine jirani.

Hata hivyo alifichua kwamba hakuwahi pita hatua ya Mkoa huku akimlaumu mwanablogu mashuhuri Denis Itumbi kwa masaibu yake.

"Nilicheza vizuri katika mashindano ya drama. Nilikuwa nafika hatua ya mkoa. Sikuwa napita hapo kwa sababu Itumbi hakutaka tupite. Alikuwa shule ya Kangaru Girls, alikuwa anafunza drama. Walikuwa wanaogopa walipotuona. Kwa kuwa  Itumbi alijuana na watu wakubwa, hatukuwa tunapita hatua ya mkoa" Itumbi alisema.

Licha ya masaibu hayo, Mwangi alisema anajivunia kusaidia kuinua hadhi ya michezo ya kuigiza ya shule aliyokuwa.

Alisema baada ya kumaliza masomo ya sekondari aliendelea kuigiza michezo ya set books kwa kuwa aliamini kwamba alikuwa na wito wa kuigiza.