Amber Ray: Sichumbii wanaume wa watu, wao ndio hunichumbia

Muhtasari

• Baada ya kushtumiwa kuchumbia wanaume waliooa, Amber Ray sasa amekana madai hayo na kusema kwamba wanaume waliioa ndio humchumbia yeye.

Amber Ray
Amber Ray
Image: INSTAGRAM

Aliyekuwa mke wa pili wa mfanyibishara wa matatu Jimal Rohosafi, Amber Ray anasema si yeye hufuata wanaume wa watu ila wanaume hao ndio humfuata. Pia alisema hana mpango wowote wa kuzaa mtoto wa pili tena huku akitoa sababu kuwa ni uhaba wa pesa.

Mwanamke huyo ambaye pia anajiongeza kama mwanamitindo ni mama wa mtoto mmoja ambaye fununu zinasema kwamba alimpata siku za nyuma akiwa bado hajachanuka sana, kabla ya kuingia katika kikaangio cha umaarufu wa mitandaoni.

Akifanya kipindi cha Q&A kupitia Instagram yake, Amber Ray aliwataka mashabiki wake wamuambie kitu kimoja ambacho wangependa aache kukifanya, ila akasisitiza hata kama hatawacha lakini wamwambie tu.

Hapo ndio mmoja alimtaka kuacha kutoka kimapenzi na wanaume wa watu naye akajibu kwamba si yeye huwafuata bali ni kinyume chake, kwa maana kwamba wanaume hao ndio humvizia na kuingia kwenye kumi na nane zake.

“Utaacha kuchumbiana na waliochukuliwa?” mmoja alimtaka.

“Siwachumbii, ni kinyume chake,” alijibu Ray.

Piamwingine alitaka kujua ni lini anapanga kupata mtoto mwingine naye akajibu kwamba hana mpango kwa sababu za kifedha, ingawa jibu hilo lilikuwa kwa njia ya mzaha kutokana na kwamba Ray anajulikana sana kwa kuserereka katika tamasha na sehemu za burudani mbalimbali.

“Mbona hutaki kuzaa tena mtoto mwingine, ikizingatiwa kuwa Gavin ashakua sasa?” mmoja alimuuliza.

“Uhaba wa pesa” alijibu Amber Ray.

Wengine walimtaka aache mambo mbalimbali kama kupakia picha za nusu uchi ambao ndio mtindo wake kwenye Instagram yake naye akajibu kwa kusema kwamba hakuzaliwa na nguo.