DeSagu aigiza YFA ya Netflix kama Young Broke and Famous

Muhtasari

• Mchekeshaji DeSagu amefurahisha wengi baada ya kufanya marudio ya kuigiza filamu ya Young Famous and African ambapo kwa upande wake ameangazia upande tofauti katika maisha.

Mchekeshaji Henry DeSagu
Mchekeshaji Henry DeSagu
Image: Facebook

Mchekeshaji Henry DeSagu hatimaye hajawafeli Wakenya kama ilivyo kawaida yake. Hii ni baada ya kufanya marudio ya maigizo ya filamu ya Young Famous and African.

Filamu hiyo inayomilikiwa na jukwaa la Netflix ilianza wiki moja iliyopita ambapo iliwahusisha watu maarufu kutoka bara la Afrika ambao pia ni matajiri kupindukia.

DeSagu ameenda kiwango kingine ambapo chini ya wiki moja tangu filamu asili kudondoshwa, yeye na timu yake wamefanya marudio ya kuigiza ambapo wameiita Young Broke and Famous.

Katika marudio hayo ya maigiza, DeSagu na kundi lake wameangazia kila kitu tofauti na kinyume kabisa na maudhui ya filamu asili ya Young Famous and African.

Kwenye filamu ya DeSagu, maudhui yanazunguka katika jinsi ambavyo watu haswa vijanaa wanaojituma kutafuta riziki ya kila siku ambapo kinyume na filamu ya Netflix ambapo watu wanaonekana kwa utajiri wakijishaua kwa magari ghali, katika hii ya DeSagu vijana wanang’ang’ana kupata afueni ya maisha kwa kutumia bajaji, maarufu tuktuk.

Filamu hiyo inayoashiria maisha ya kung’ang’ana na ya chini, wahusika wanajifurahisha sana kuzungumza lugha ya sheng ambayo ni maarufu sana katika mazingira ya mijini nchini kenya, kinyume na filamu ya Netflix ambapo wahusika wanajikosha na ueledi wa kizungu ili kuonesha utajiri wao.