"Ndoa ni ulaghai!" Mwanaume aeleza kwa majonzi baada ya ndoa ya miaka 30 kuvunjika

Muhtasari

• Baada ya miaka 30 ya ndoa na watoto wanne, nikagundua mwanamke niliyempenda na bado ninampenda alikuwa akipenda sana mwanaume mwingine - Baron

• Ina maana nimepoteza miaka 30 ya maisha yangu na shetani, Ndoa ni ulaghai - Baron.

Mwanaume aliyevunjika moyo wa mapenzi
Mwanaume aliyevunjika moyo wa mapenzi
Image: THE STAR, MOSES SAGWE

Mwanaume mmoja mtumizi wa mtandao wa Twitter ameelezea kwa uchungu na ukakasi mno jinsi ndoa yake ilivyovunjika. Ndoa ambayo aliyojitoa mhanga kwa miongo mitatu, nazungumzia miaka 30 na kuvunjika tu kwa siku moja!

Gumzo hilo kuhusu kuvunjika kwa ndoa lilianzishwa na mtumizi mmoja kwa jina David Hundeyin aliyesema kwamba mwanaume mmoja ndoa yake ilisambaratika baada ya kuijenga kwa miaka 37 na mwanamke ambaye alishindwa kumpenda licha ya kuwa na watoto watano naye.

Hundeyin alieleza kwamba mwanaume huyo alikufa kabla ya mkewe baada ya kuteseka na watoto kutoroshwa kutoka kwake.

Hapo ndipo watu mbalimbali walijimwaya na kuzungumzia matatizo katika ndoa zao ambazo walikuwa wamewekeza muda, fikra na mawazo yao kwa miaka mingi.

Jamaa kwa jina Baron alizungumza kwa kusema kwamba alijipata katika kisa kama hicho na kueleza kwamba yake ilifikia kikomo baada ya miaka 30 ya kujituma na kuwekeza muda wake kwa mtu ambaye mwisho wa siku alimuona kama hayawani.

“Mimi pia nilijipata kwa kisa kama hicho, ninapitia mengi sasa hivi, baada ya miaka 30 ya ndoa na watoto wanne, nikagundua mwanamke niliyempenda na bado ninampenda alikuwa akipenda sana mwanaume mwingine. Niliondoka nyumbani kwake na kujikodisha chumba sasa, watoto wangu bado wanakuja kuniona kila siku ofisini kwangu kwa pesa zao za utunzaji. Nina miaka miwili tangu niondoke nyumbani pale, ameolewa na mwanaume yule yule niliyemfumania, alidai yuko na yule kijana tangu siku zao za shule ya sekondari mpaka sasa. Ina maana nimepoteza miaka 30 ya maisha yangu na shetani na Frenemie. Ndoa ni ulaghai,” Baron alieleza kwa ukakasi uliopitiliza.