Mulamwah afichua ameweka akiba ya zaidi ya Shilingi Milioni kwa ajili ya bintiye

Muhtasari

•Mulamwah  alionyesha salio la benki la Ksh1, 011, 715 ambazo alisema amewekea binti yake Keilah Oyando.

•Mulamwah alisema anakusudia kumpatia Keilah pesa hizo wakati atakapofikia umri wa kuwajibika.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah amefichua kuwa kufikia sasa ameweka akiba ya zaidi ya shilingi milioni moja kwa ajili ya bintiye wa miezi tisa.

Mulamwah  akiwa kwenye mahojiano na Plug TV alionyesha salio la benki la Ksh1, 011, 715 ambazo alisema amewekea binti yake Keilah Oyando.

Hata hivyo alifichua kuwa mara kwa mara huwa anachukua kiasi fulani kutoka kwa akiba hiyo ikitokea anazihitaji.

"Huwa natumia nikiona nataka kutumia lakini ni pesa iko hapo, ni yake. Mimi sioni kama kuna kitu nakosa. Kama ni kuku nataka nitakula. Nikitaka kuenda likizo nitaenda. Hii pesa iko hapa ni yake, kwangu bora nikule nilale imetosha. Chochote kingine sitaki," Mulamwah alisema.

Image: PLUG TV

Mchekeshaji huyo alieleza kuwa anakusudia kumpatia Keilah pesa ambazo atakuwa ameweka kwa ajili yake wakati atakapofikia umri wa kuwajibika.

Alifichua kuwa alianza kuweka akiba kwa ajili ya binti yake hata kabla hajazaliwa.

"Hii ni pesa yake. Akikua, kusoma na mahitaji muhimu ndio kazi ya pesa hiyo. Sijui itakuwa lini, labda wakati huo yeye atakuwa na pesa nyingi kuniliko. Jambo ni kuwa tayari tu," Alisema.

Mchekeshaji huyo pia ameweka wazi kuwa kwa sasa hataki kujihusisha na mahusiano yoyote ya kimapenzi.

Mulamwah amesema kuwa kwa sasa anaangazia biashara na kazi zake huku akilenga kujipatia utajiri zaidi.

"Sitaki kujisumbua na mambo ambayo hayaongezi thamani sana katika maisha. Wakati mwingine huwa yanamaliza mtu nguvu. Nimeona ni vizuri kusimamisha kidogo," Mulamwah alisema.