Hongera! Willis Raburu amvisha pete ya uchumba mpenzi wake kutoka Uganda, Ivy Namu

Muhtasari

•Raburu alipiga hatua Jumapili katika karamu iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mwanawe Mali.

•Raburu na Namu wamekuwa kwenye mahusiano kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

Ivy Namu na Willis Raburu katika karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wao.
Ivy Namu na Willis Raburu katika karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wao.
Image: INSTAGRAM

Hatimaye mtangazaji maarufu Willis Raburu amemvisha mpenzi wake Ivy Namu pete ya uchumba.

Mtangazaji huyo mwenye umri wa miaka 35  alipiga hatua hiyo siku ya Jumapili katika karamu iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mwanawe Mali.

Mali ambaye ni kifungua mimba cha wapenzi hao alitimiza mwaka mmoja.

Huku karamu hiyo iiyohudhuriwa na wageni waalikwa wachache ikiendelea, Raburu alisimama mbele ya mpenzi wake akiwa ameshika kitu kilichofanana na ua la waridi jekundu kwenye mkono mmoja na kipaza sauti kwenye mkono mwingine.

"Wewe ni mpenzi wangu, wewe ni kila kitu kwangu na itanipa furaha kubwa.." Raburu alimwambia mpenziwe kabla ya kupiga goti na kufungua 'ua' alilokuwa ameshika.

Ndani ya ua hilo bandia kulikuwa na pete ya uchumba.

"... kama wewe Ivy Namulindwa unaweza kuwa mke wake.. tunahitaji jibu," Aliendelea kusema mtangazaji huyo huku akiwa amepiga goti mbele ya Namu.

Namu ambaye alionekana mwenye  bashasha kupitiliza hakusita kukubali ombi hilo la ndoa ambalo huenda lilimpata kwa mshangao.

Wageni waliokuwa wamejumuika pale walisherehekea hatua hiyo na kuwapongeza wawili hao ambao hivi karibuni huenda wakafunga pingu za maisha.

Haya yanajiri takriban mwezi mmoja baada ya wachumba hao wawili kutangaza habari kuhusu ujauzito wa mtoto wao wa pili.

Raburu na Namu wamekuwa kwenye mahusiano kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili na tayari wana mtoto mmoja wa kiume ambaye alizaliwa mwaka jana.

Namu ni mzaliwa wa Uganda na alikuja kujulikana zaidi nchini Kenya baada ya kujitosa kwenye mahusiano na Raburu.

Wawili hao walianza kuchumbiana kipindi kifupi tu baada ya Raburu kutengana na aliyekuwa mke wake Marya Prudence.

Wawili hao walitengana mwaka wa 2020 baada ya kuwa kwa ndoa kwa takriban miaka mitatu. Waliwahi kubarikiwa na mtoto mmoja lakini kwa bahati mbaya akaaga.