"Siamini alirogwa!" Babake muuguzi aliyekufa maji nchini Canada azungumzia kifo cha bintiye

Hellen Wendy hatimaye alizikwa nyumbani kwao Kisii takriban miezi miwili baada ya kifo chake.

Muhtasari

•Mwili wa Wendy ulizikwa Jumatano nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Getare-Misesi, eneo bunge la Bomachoge Chache, Kaunti ya Kisii. 

•Licha ya utata uliozingira kifo cha bintiye, Nyabuto alisema kuwa anaamini mtot huyo wake wa kwanza alikufa kifo cha kawaida.

Image: FACEBOOK// HELLEN WENDY

Hellen Wendy Kemunto, muuguzi wa Kenya ambaye alikufa maji alipokuwa akiogelea kwenye bwawa nchini Canada hatimaye alizikwa.

Mwili wa Wendy ulizikwa Jumatano nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Getare-Misesi, eneo bunge la Bomachoge Chache, Kaunti ya Kisii. 

Hali ya huzuni ilitanda huku wanafamilia, marafiki, majirani na watu wengine wa karibu ambao walihudhuria hafla ya mazishi wakimuaga kwaheri mwanadada huyo mdogo kwa mara ya mwisho.

"Tulipopata habari kuhusu kifo cha mtoto wetu Hellen tulishtuka sana. Tulishindwa tutafanya nini lakini nikaomba Mungu atupatie usaidizi na akasikia kwa kweli akasikia maombi yangu," babake Wendy, John Nyabuto, alisema huku akiwashukuru waombolezaji waliokuwa wamefurika nyumbani kwake.

Huku akitoa hotuba yake, Bw Nyabuto alisema marehemu alikuwa la familia na kubainisha kuwa kifo chake ni pigo kubwa sana kwao.

Licha ya utata uliozingira kifo cha bintiye, Nyabuto alisema kuwa anaamini mtot huyo wake wa kwanza alikufa kifo cha kawaida.

"Mimi siwezi nikalaumu mtu yeyote. Mimi siamini uchawi. Ndio uchawi upo, lakini kwa kesi hii ya mtoto wangu siamini kama kuna mtu ambaye alimroga!," alisema.

Alibainisha kuwa bintiye amekuwa akiishi Canada kwa zaidi ya miaka 5 na haamini kuwa kuna mchawi aliyeenda hadi huko kumroga bintiye.

"Pengine aliteleza kule majini, pengine alipata shinikizo la misuli akaanguka kule majini. Mipango ya Mungu hatuwezi kuikosoa," alisema.

Nyabuto alitoa shukran zake kwa Maulana kwa kusimama na familia yake tangu wakati bintiye alipofariki takriban miezi miwili iliyopita.

Hata hivyo alieleza wasiwasi wake kuhusu ustawi wa watoto wake wengine watano kwa kuwa Wendy alikuwa tumaini lao kuu.

Wendy alifariki mnamo Agosti 18 wakati akishirikisha marafiki wake kwenye kipindi cha moja kwa moja kwenye Facebook.