Diamond alia kuwa mpweke baada ya kuthibitisha kutengana na Zuchu

Bosi huyo wa WCB aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena.

Muhtasari

•Diamond alithibitisha kuvunjika kwa mahusiano yake na Zuchu siku ya Jumamosi baada ya wawili hao kudokeza uhusiano wao umeingiwa na dosari.

•Diamond alibainisha kuwa yeye na Zuchu wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa  kati yao.

wamethibitisha kutengana
Diamond Platnumz na Zuchu wamethibitisha kutengana
Image: INSTAGRAM

Diamond Platnumz ameomba kukaribishwa katika ulimwengu wa watu wapweke baada ya kuachana na aliyeaminika kuwa mpenzi wake, Zuchu.

Bosi huyo wa WCB alithibitisha kuvunjika kwa mahusiano yake na bintiye Khadija Kopa siku ya Jumamosi baada ya wawili hao awali kuonyesha vidokezo kadhaa kwamba uhusiano kati yao umeingiwa na dosari.

"Nipokee kwenye ufalme wako wa walio wapweke kaka," Diamond alimwandikia meneja wa WCB Ricardo Momo baada ya kuthibitisha yuko single.

Katika taarifa yake ya Jumamosi jion kwenye ukurasa wake wa Instagram, staa huyo wa Bongo aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena.

Diamond alibainisha kuwa yeye na msanii huyo wake wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa yasiyovunjika kati yao.

"Kwa pamoja na Zuhura tunaomba tuwataarifu ya kwamba, kwa sasa sisi ni dada na kaka na si wapenzi kama ilivyokuwa ikidhaniwa ama wengine kujua.. Mnaruhusiwa wachumba na wake ama waume kama tutawaridhia," alisema.

Diamond aliongeza, "Lakini muwe na vibarua vinavyoeleweka  sio mje kutuchuna, maana atuhongi hovyo."

Siku ya Ijumaa, Zuchu aliibua wasiwasi juu ya hali ya mahusiano yao kufuatia chapisho lake kwenye mtandao wa Snapchat.

Mwimbaji huyo wa kibao 'sukari' alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.

"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'

Zuchu hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu taarifa hiyo mpya na kuwaacha mashabiki wake wakiwaza na kukisia tu kilichofanyika.

Aidha, binti huyo wa Khadija Kopa pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond kwenye mtandao wa Instagram.

Diamond aliendelea kuongeza wasiwasi miongoni mwa mashabiki wao huku akichapisha ujumbe wa kimafumbo kwenye ukurasa wake wa Instagram ambao ulionekana kuzungumzia uhusiano wake.

Bosi huyo wa WCB alikubaliana na maneno ya meme iliyosomeka, “Muweke mpenzi wako mbele na umuone akianza kukutumia vibaya.

Kwa chapisho hilo, Diamond alionekana kudokeza kuwa Zuchu amekuwa akijinufaisha na yeye kwa sababu ya mapenzi yake makubwa kwake.

Takriban wiki mbili zilizopita, Diamond aliwasisimua wanafamilia wake huku akimtambulisha msanii huyo wake kama mke wake wakati wa karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya dada yake mkubwa Esma.