Harmonize ammwagia sifa kemkem mzazi mwenza wa Diamond, amhimiza abaki single

"Shukran sana, najua uko single kweli. Baki hapo," alimwambia Mobetto.

Muhtasari

•Harmonize alishangaa kwa nini wanaume wamekuwa hawamsumbui na kulilia penzi lake licha ya jinsi anavyopendeza.

•Harmonize alibainisha kwamba anafahamu mwanamitindo huyo hana mchumba na kumhimiza hata asihangaike kutafuta yeyote.

Harmonize na Hamisa Mobetto
Image: INSTAGRAM

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amemimina sifa kemkem kwa mwanamitindo wa Tanzania Hamisa Mobetto.

Siku ya Jumapili jioni, bosi huyo wa Kondegang alichapisha video ya Mobetto akifurahia wimbo wake 'Single Again' na kuambatanisha na ujumbe mrefu mtamu wa sifa kwa mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz.

"Niseme nini? Kweli, yeye ndiye malkia aliyepunguzwa sana katika mji wangu wa nyumbani?" Konde Boy alihoji kwenye Instagram.

Harmonize alibainisha kuwa mama huyo wa watoto wawili ndiye mwanamke anayefuatiliwa zaidi kwenye mtandao wa Instagram nchini Tanzania akiwa na mashabiki zaidi ya milioni 10. Alishangaa kwa nini wanaume wamekuwa hawamsumbui na kulilia penzi lake licha ya jinsi anavyopendeza.

"Sisi huwa tunawalia wasiofaa. Hakuna anayejivunia yeye. Wanamficha ficha daah," alisema.

Mwimbaji huyo wa zamani wa lebo ya WCB hata hivyo alimhakikishia Hamisa Mobetto kwamba anajivunia yeye.

“Najua haupo tayari kuwa na mtu kwa sababu ukitaka unaweza kuwa na mtu yeyote kwenye gemu , ukimtoa Konde Boy,” alisema.

Harmonize alibainisha kwamba anafahamu mwanamitindo huyo hana mchumba na kumhimiza hata asihangaike kutafuta yeyote.

"Shukran sana, najua uko single kweli. Baki hapo,"

Aliambatanisha ujumbe huo na video ya Hamisa akijiburudisha kwenye klabu huku akicheza na wimbo wa 'Single Again'.

Hatua ya Harmonize inaonekana kuwa ya utata kwa kuwa Hamisa Mobetto anajulikana kuwahi kuchumbiana na bosi wake wa zamani ambaye sasa ni mpinzani wake mkubwa kwenye tasnia ya muziki Bongo, Diamond Platnumz.

Mobetto alikuwa kwenye mahusiano na bosi huyo wa WCB kwa kipindi kifupi na wanaaminika kuwa na mtoto mvulana pamoja, Dylan Abdul Naseeb. Hata hivyo kumekuwa na mvutano kati ya wawili hao kuhusu mtoto huyo.

Mwaka jana, mwanamitindo huyo alilalamika kwamba Diamond amemtelekeza mtoto na kudai hajui sababu yake. Hii ni baada ya mzazi huyo mwenzake kutomsherehekea mtoto huyo akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

"Kusema ukweli sifahamu kwa nini nadhani hilo swali ni vizuri sana akiulizwa yeye mwenyewe binafsi mi ntakua sina majibu na mi si mtu ambaye anauliza nadhani ni maamuzi tu mtu unaamka tu asubui unaamua," alisema.

Diamond amekuwa akijitenga  wazi na mtoto wa Mobetto huku akiwasherehekea watoto wake wengine na Zari na Tanasha.