Amber Ray afichua kiasi kikubwa cha hela anachotumia kila mwezi, ajigamba analipa kodi ya 350k

Amesema huwa anahitaji takriban Ksh300,000 wakati wowote anapotaka kwenda kujiburudisha na marafiki.

Muhtasari

•Mwanasholaiti Faith Makau almaarufu Amber Ray amefichua kuwa kwa kawaida yeye hutumia wastani wa Ksh1.5 milioni kwa mwezi.

•Alifichua hawana mpango wa kukaa sana katika nyumba hiyo ghali kwani wako katika harakati za kujenga nyumba ya ndoto zao.

KENNEDY RAPUDO WAKIWA NA AMBER RAY.
KENNEDY RAPUDO WAKIWA NA AMBER RAY.
Image: INSTAGRAM// AMBER RAY

Mwanasholaiti mashuhuri wa Kenya Faith Makau almaarufu Amber Ray amefichua kwamba kwa kawaida yeye hutumia wastani wa Ksh1.5 milioni kwa mwezi.

Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, mama huyo wa watoto wawili alidai kwamba huwa analipa kodi ya Ksh350,000 kwa mwezi kwa nyumba ya kupanga ambayo yeye na familia yake walihamia mwaka uliopita.

"Nitasema bajeti yangu ni milioni 1.5, kuwa upande salama.. kodi yangu ni 350k," Amber Ray alisema siku ya Ijumaa.

Hata hivyo alifichua kuwa hawana mpango wa kukaa kwa muda mrefu katika nyumba hiyo yenye kodi ya gharama kubwa kwani yeye na mume wake Kennedy Rapudo wako katika harakati za kujenga nyumba ya ndoto zao.

“Unajua saa zingine unatafuta pesa kwa ugumu, mbona usifurahie maisha yako wakati huohuo. Tukasema maadam tunaishi Nairobi kwanini tusipende nyumba. Yenye tunahisiu tumefurahi. Ni kwa muda tu, sio eti tutaishi pale milele. Tuko na mpango wa kujenga,” alisema.

Mama huyo wa watoto wawili pia alijigamba kwamba kwa kawaida huwa anahitaji takriban Ksh300,000 wakati wowote anapotaka kwenda kujiburudisha na marafiki.

“Yote ni ile nistarehe, naweza kutumia yote. Unajua sisi tumezoea kunawa na pombe, champagne,” alisema.

Amber Ray ni miongoni mwa wanawake maarufu zaidi nchini na anajulikana kwa mtindo wake wa maisha wenye utata, ghali na wa kipekee.

Mapema mwaka huu, mwanasosholaiti huyo mrembo anayeonekana kuwa na maisha laini na mume wake, Kennedy Rapudo  waliwafurahisha mashabiki wao kwa kushiriki video ya makazi yake mapya ya kifahari.

Amber Ray alionyesha nyumba yake kamili na iliyo na lifti. Katika video hiyo, alishuka kutoka kwenye lifti, ambayo ilienda moja kwa moja kwenye sebule yake, akitembea hadi kwenye ukumbi akiwa na glasi ya mvinyo mkononi.