Diamond ajipatia jumba la kifahari karibu na aliyekuwa mpenzi wake, Zari Hassan (+picha)

"Ni vizuri sana kurudi nyumbani!" Diamond alisema.

Muhtasari

•Diamond alionyesha  jumba hilo kubwa la kifahari lililo Johannesburg kupitia ukurasa wake wa Instagram

•Baadhi ya washiriki wa timu yake ya muziki walionekana wakistarehe katika vyumba tofauti vya kulala.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Siku ya Jumanne, staa wa Bongo Diamond Platnumz kwa mara ya kwanza alionyesha nyumba yake ya kifahari iliyo Afrika Kusini.

Msanii huyo mzaliwa wa Tanzania alionyesha  jumba hilo kubwa la kifahari lililo Johannesburg kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mbali na kuwa na vyumba vingi na samani za kupendeza, nyumba hiyo pia ina bwawa la kuogelea ndani yake.

"Ni vizuri sana kurudi nyumbani!" aliandika chini ya video iliyoonyesha nyumba hiyo ambayo alipakia kwenye Instastori zake.

Katika video hiyo, baadhi ya washiriki wa timu yake ya muziki walionekana wakistarehe katika vyumba tofauti vya kulala.

Diamond alitumia fursa hiyo kutangaza kuwa baada ya kupumzika kule Afrika Kusini kwa muda wataendelea na ziara yao ya muziki katika mataifa mbalimbali.

"SA kwa siku kadhaa! Kisha Paris , kisha London, kisha shoo ya Wembley OVO Rena, kisha Malawi," alitangaza.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na ripoti kuwa staa huyo wa Bongo mwenye umri wa miaka 32 anamiliki jumba la kifahari Afrika Kusini. Msanii huyo hata hivyo hakuwahi kuonyesha jumba hilo kikamilifu hapo awali.

Tazama picha za jumba la Diamond hapa:-

Afrika Kusini ndiko anakoishi mpenzi wake wa zamani Zari Hassan pamoja na watoto wao wawili, Tiffah Dangote na Prince Nillan.

Mwanasoshalaiti huyo kutoka Uganda amekuwa akiishi huko kwa miaka kadhaa ili kuweza kufuatlia biashara zake kwa karibu.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa Diamond aliamua kutafuta makao huko Afrika Kusini ili kupata fursa ya kuwa na kipindi kizuri pamoja na familia yake kila mara anapofanya ziara katika nchi hiyo.

Miezi  kadhaa iliyopita baba wa kambo wa Diamond, Uncle Shamte alifichua kuwa bosi huyo wa WCB amefanikiwa kununua viwanja 67 na kujenga  makumi ya nyumba  katika maeneo mbalimbali Tanzania.

"Naseeb ana nyumba nyingi. Nyumba kama 67 . Mimi binafsi nina miaka  mitano kwenye familia, sasa nasimamia nyumba ya 61. Hatujipi sifa kusimamia nyumba lakini tunapozungumza sasa hivi hivyo ndivyo uwezo wake ulivyo" alisema katika mahojiano na Wasafi Media

Aliweka wazi kwamba nyumba hizo za mwanamuziki huyo ni za kupangisha wala sio zake  mwenyewe kukaa.