Hamisa Mobetto afunguka sababu za kumficha mpenzi wake hadharani

Mobetto alieleza kuwa kwa kawaida huwa hathamini kuyaanika mahusiano yake hadharani.

Muhtasari

•Alidai kuwa wakati mtu anapoamua kuanika mahusiano yake hadharani, basi yanakoma kuwa ya kibinafsi na kuwa ya umma.

•Alibainisha kuwa kufichua mahusiano hadharani mara nyingi huwafanya  watu waache kujizingatia na badala yake kuzingatia penzi.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Msanii maarufu wa Bongo Hamisa Mobetto amekanusha madai kuwa amekuwa akimficha mpenzi wake wa sasa kwa kuhofia kupokonywa.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano, Mobetto alieleza kuwa kwa kawaida huwa hathamini kuyaanika mahusiano yake hadharani.

Alidai kuwa wakati mtu anapoamua kuanika mahusiano yake hadharani, basi yanakoma kuwa ya kibinafsi na kuwa ya umma.

"Mimi naamini kama kitu ni chako na Mungu amepanga, basi kitakufikia na hakitakuwa cha kuibiwa. Siamini kama mwanaume anaweza kuibiwa... Sio kama namficha. Mimi na yeye tuko vizuri katika mapenzi yetu. Tunakula, tunatembea pamoja, yaani tuko vizuri," Hamisa alisema.

Pia alidai kuwa sio sawa kwake kuendelea kuwatambulisha wapenzi wapya kila wanapokuja katika maisha yake huku akibainisha kuwa tayari yeye ni mama wa watoto wawili wenye baba tofauti.

"Tukifika mbele huko kama Mwenyezi Mungu alimuandikia kuwa mume wangu basi huenda watu wataanza kumjua. Lakini sasa hivi kama tukiachana? nikipata mwingine tena nimtambulishe," Alisema.

Aidha alibainisha kuwa kufichua mahusiano hadharani mara nyingi huwafanya  watu waache kujizingatia na badala yake kuzingatia penzi.

Licha ya kutomtambulisha mpenzi wake wa sasa hadharani, Hamisa ameweka wazi kuwa kwa sasa anaogelea kwenye dimbwi la mahaba anayopata kutoka kwake.

Amemtaja mpenzi huyo wake mpya kama "mwanaume mzuri sana."

Kufikia sasa Mobetto amewahi kuwa kwenye mahusiano kadhaa na hata kupata watoto na wapenzi wake wawili wa zamani.

Mtoto wake wa kwanza, Fantasy Majizzo alizaliwa 2015 wakati alipokuwa kwenye mahusiano na Bw  Francis Ciza 'Majizo'. 

Dylan Abdul Naseeb ni mtoto wa pili wa Mobetto ambaye alizaa pamoja na staa wa Bongo Diamond Platnumz mnamo Agosti 8, 2017.

Kwa kipindi kirefu mwanamitindo huyo amedaiwa kuwa kwenye mahusiano na staa wa HipHop kutoka Marekani Rick Ross.

Mara nyingi hata hivyo Mobetto amejitokeza kuweka wazi kuwa uhusiano wake na mwanamuziki huyo ni wa kikazi tu.