Hamisa Mobetto azungumzia mipango kuongeza mtoto na mpenziwe

Amefichua kuwa mpenziwe ndiye mwanaume pekee aliyewahi kuchumbiana naye ambaye hajaomba kuzaa naye.

Muhtasari

• Mobetto aliweka wazi kuwa hajawahi kujadili suala la mtoto na mpenzi wake asiyejulikana katika kipindi ambacho wamekuwa kwenye mahusiano.

•Mobetto hakufutilia mbali uwezekano wa kuwahi kupata mtoto na mpenzi huyo wake katika siku za usoni za mahusiano yao ambayo yamesalia siri.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Mwanamitindo maarufu wa Bongo Hamisa Hassan Mobetto amefichua kuwa mpenzi wake wa sasa ndiye mwanaume pekee aliyewahi kuchumbiana naye ambaye hajaomba kuzaa mtoto naye. 

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano, Mobetto aliweka wazi kuwa hajawahi kujadili suala la mtoto na mpenzi wake asiyejulikana katika kipindi ambacho wamekuwa kwenye mahusiano.

Vilevile alibainisha kuwa kwa sasa ameridhika na watoto wawili ambao tayari anao.

"Kwa sasa hivi siko pia kwenye utayari wa kuongeza mtoto. Sasa hivi niko na watoto wawili, wa kike na wa kiume," Mobetto alisema

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz hata hivyo hakufutilia mbali uwezekano wa kuwahi kupata mtoto na mpenzi huyo wake katika siku za usoni za mahusiano yao ambayo yamesalia siri.

"Sasa hivi najiangazia mwenyewe zaidi. Huko mbele labda baada ya kufunga pingu za maisha kama Mwenyezi Mungu ameniandikia ndio ninaweza kuongeza mtoto mwingine, lakini sio kwa sasa," Alisema.

Kuhusu suala la kumficha mpenziwe, Mobetto alieleza kuwa kwa kawaida huwa hathamini kuyaanika mahusiano yake hadharani.

Alidai kuwa wakati mtu anapoamua kuanika mahusiano yake hadharani, basi yanakoma kuwa ya kibinafsi na kuwa ya umma.

"Mimi naamini kama kitu ni chako na Mungu amepanga, basi kitakufikia na hakitakuwa cha kuibiwa. Siamini kama mwanaume anaweza kuibiwa... Sio kama namficha. Mimi na yeye tuko vizuri katika mapenzi yetu. Tunakula, tunatembea pamoja, yaani tuko vizuri," Hamisa alisema.

Pia alidai kuwa sio sawa kwake kuendelea kuwatambulisha wapenzi wapya kila wanapokuja katika maisha yake huku akibainisha kuwa tayari yeye ni mama wa watoto wawili wenye baba tofauti.

"Tukifika mbele huko kama Mwenyezi Mungu alimuandikia kuwa mume wangu basi huenda watu wataanza kumjua. Lakini sasa hivi kama tukiachana? nikipata mwingine tena nimtambulishe," Alisema.

Aidha alibainisha kuwa kufichua mahusiano hadharani mara nyingi huwafanya  watu waache kujizingatia na badala yake kuzingatia penzi.

Licha ya kutomtambulisha mpenzi wake wa sasa hadharani, Hamisa ameweka wazi kuwa kwa sasa anaogelea kwenye dimbwi la mahaba anayopata kutoka kwake.

Amemtaja mpenzi huyo wake mpya kama "mwanaume mzuri sana."