"Ilitokea!" Dadake Vanessa Mdee afunguka kuhusu tukio ambapo alionekana akiogelea na Diamond

Tukio hilo liliibua hisia ya mahusiano ya kimapenzi kati ya Mars na Diamond.

Muhtasari

•Mars ambaye ni dada mdogo wa Vanessa Mdee alisema ni tukio ambalo lilijitokeza tu na halikuwa limepangwa.

•Marioo aliwahi kujitokeza kukiri kuwa video ya Mars akiogelea na Diamond iliuumiza sana moyo wake.

Image: INSTAGRAM// MIMI MARS NA DIAMOND

Msanii wa Bongo Mimi Mars amefunguka kuhusu tukio la 2020 ambapo alionekana akijivinjari kwenye bwawa la kuogelea pamoja na Diamond Platnumz.

Akiwa kwenye mahojiano na Millard Ayo, Mars ambaye ni dada mdogo wa Vanessa Mdee alisema ni tukio ambalo lilijitokeza tu na halikuwa limepangwa.

Alifichua kwamba kuna kazi ambayo alikuwa anafanya pale nyumbani kwa Platnumz wakati hilo lilijitokeza.

"Ilikuwa sio video. Ilitokea tu, nahisi naweza nikasema hivo. Sikuenda kumtembelea, nilikuwa na kazi nafanya lakini ilitokea," Mimi Mars alisema.

Mwezi Septemba, 2020 video ambayo ilienezwa kwenye mitandao ya kijamii iliwaonyesha Diamond na Mimi Mars wakijivinjari pamoja kwenye bwawa la kuogelea.

Tukio hilo liliibua hisia ya mahusiano ya kimapenzi kati ya wasanii hao wawili.

Hapo awali Diamond alikuwa amepakia video ya Mars  akinengua kiuno kwa wimbo wake  'Cheche' na kuandika;

“Mi nakapendaga haka katoto…. Sema sjui ata Tyming naikoseaga wapi Mwana wa Dangote… Doh! @mimi_mvrs11 ….. #CHECHE,”

Baadae hata hivyo Mars alijitokeza kupuuzilia mbali madai kuwa yupo kwenye mahusiano na bosi huyo wa Wasafi.

Takriban miezi miwili iliyopita, Marioo  alikiri video ya Mars akiogelea na Diamond iliuumiza sana moyo wake.

Msanii huyo akiwashirikisha mashabiki wake kwenye kipindi cha maswali na majibu alifichua kuwa hilo ndilo tukio ambalo limewahi kuumiza zaidi maishani.

"Yapo mengi ila nilivoonaga ile klipu video ya rafiki yangu wa kike anaogelea kwenye pool la broo ilinigusa nayo ile," Marioo alimjibu shabiki aliyeuliza kuhusu tukio ambalo limewahi kumuumiza zaidi.

Marioo anafahamika kuwa rafiki mkubwa wa Mars na kwa kipindi kirefu kumekuwa na madai ya mahusiano kati yao.

Mwezi uliopita dadake Mdee aliweka wazi kuwa hakuna mahusiano yoyote ya kimapenzi kati yake na Marioo.

"Mimi na Marioo hatupo kwenye mahusiano. Tuna mahusiano ya kirafiki ambayo ni mazuri. Nahisi hicho dicho kinasababisha watu kusema tupo kwenye mahusiano," Mars alisema katika mahojiano na Wasafi Media.

Mars aliweka wazi kuwa tayari yupo kwenye mahusiano mengine na mwanaume ambaye sio mtu maarufu.

Aidha alibainisha kuwa hakujua kuwa tukio la yeye kuogelea na Diamond lingemuumiza moyo Marioo na hivyo basi hakuona haja ya kujieleza wakati ule.

"Sidhani kama nilihitaji kumweleza chochote. Sikujua chochote muda huo eti angeumia. Mimi mwenyewe nilikuja kujua juzi alipoweka kwenye Instastori zake. Hakuwahi kuniambia," Alisema.

Mars hata hivyo aliweka wazi kuwa hakukerwa na hatua ya Marioo kufunguka kuhusu hisia zake kufuatia tukio hilo.