Terence Creative aomba radhi kwa kula chakula huku akiendesha gari barabarani

Muhtasari

•Video ambayo alipakia ilionyesha akiwa amekalia kiti cha dereva huku akifurahia sahani ya ugali kwa nyama.

•Terence amebainisha kwamba hakuwa anaendesha kwa mwendo kasi na hakukuwa na watoto wowote mle ndani wakati video hiyo iliporekodiwa. 

Image: INSTAGRAM// TERENCE CREATIVE

Mchekeshaji Terence Creative amelazimika kuwaomba  Wakenya radhi baada ya kupakia video inayoonyesha akila huku akiendesha gari.

Video ambayo mchekeshaji huyo alichapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ilionyesha akiwa amekalia kiti cha dereva huku akifurahia sahani ya ugali kwa nyama.

Huku akiomba msamaha, Terence amewashauri wafuasi wake kutoiga tabia hiyo na kubainisha kuwa inahatarisha maisha. Aidha aliahidi kurekebisha tabia hiyo na kuwa balozi wa usalama wa barabarani.

"Ningependa kuomba radhi na kuwaomba msiige tabia hii kwani inaweza kuwaweka hatarini na kuhatarisha maisha ya watu walioko ndani ya gari, samahani kwa hilo na muwe salama, naahidi kuwa balozi na mtetezi wa usalama na uendesha gari kama inavyoonyeshwa na sheria za kenya na zile za NTSA," Alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mchekeshaji huyo pia alibainisha kuwa hakuwa anaendesha kwa mwendo kasi na hakuna watoto wowote ambao walikuwa mle ndani ya gari wakati video hiyo iliporekodiwa. 

"Tulikuwa tukiendesha gari mwendo wa kilomita 30 kwa saa, walakini hii haihalalishi kitendo changu .Kwa mara nyingine tena naomba radhi kwa onyesho hilo,"  Alisema

Kile ambacho huenda kilikusudiwa kuwaburudisha wafuasi wake hata hivyo hakikuishia vyema kwake. Wanamitandao wengi walijitokeza kumkosoa huku baadhi yao wakitaka Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) kuchukua hatua.

Shabiki mmoja alisema; "Huku ni kutowajibika sana, kuwaweka madereva wengine hatarini. Terence kama mtu mashuhuri na ambaye vijana wengi wanakufuatilia, huu sio mfano mzuri."

" Shabiki mwingine aliandika; "Kaka, weka gari kando ya barabara, kula kisha endelea na safari. Kila unachofanya ni kichafu na hatari."

Baada ya kupokea jumbe nyingi za ukosoaji, baba huyo wa watoto watatu aliifuta video hiyo kabla ya kuchukua hatua ya kuomba msamaha.