Kajala avunja kimya kuhusu binti yake Paula kutoka kimapenzi na Marioo

"Ukimuuliza anakwambia hayuko kwenye mahusiano lakini picha kila saa anaziposti," Kajala alilalamika.

Muhtasari

•Kajala aliweka wazi kuwa pia yeye anapata tetesi za mahusiano ya wawili hao kwenye mitandao ya kijamii.

•Kajala alibainisha kuwa bintiye sasa ni mtu mzima na yuko katika nafasi ya kufanya maamuzi yake mwenyewe.

Kajala, Marioo, Paula
Image: HISANI

Muigizaji maarufu wa filamu bongo Frida Kajala Masanja amekiri kwamba hana uhakika iwapo binti yake Paula Paul Kajala yupo kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwimbaji Omary Mwanga almaarufu Marioo.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize aliweka wazi kuwa pia yeye anapata tetesi za mahusiano ya wawili hao kwenye mitandao ya kijamii.

"Sijui. Kwa kweli sijui chochote. Picha naziona tu kama wananchi wengine," alisema.

Kajala alisema kuwa binti yake huyo mwenye umri wa miaka 20 amekuwa akikanusha kuwa kwenye mahusiano kila anapomuuliza.

Muigizaji huyo alilalamika kuwa licha ya bintiye kukana kuwa kwenye mahusiano, ameonyesha dalili wazi za kuchumbiana na Marioo.

"Ukimuuliza anakwambia hayuko kwenye mahusiano lakini picha kila saa anaziposti," Kajala alilalamika.

Hata hivyo, alibainisha kuwa bintiye sasa ni mtu mzima na yuko katika nafasi ya kufanya maamuzi yake mwenyewe.

Katika siku kadhaa za hivi majuzi, mwimbaji Marioo amekuwa akionekana akijivinjari na mwanamitindo Paula Kajala.

Haijabainika iwapo wawili hao wanatoka kimapenzi lakini kwa hakika wamekiri kupendana. Siku chache zilizopita, Marioo alisifu urembo wa mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 na kubainisha kuwa anampenda.

"Imagine mtoto mbichi kama huyu alafu anakupenda.. @therealpaulahkajala #ananipenda inakuja hivi karibuni," Marioo aliandika chini ya video ya Tiktok ya Paula akicheza wimbo wake mpya 'Ananipenda.' 

Huku akijibu kwenye chapisho hilo la Instagram, binti huyo wa muigizaji Kajala Masanja alisema laiti wangekutana awali.

"Natamani ningekutana nawe awali," aliandika na kuambatanisha na emoji zilizoashiria mahaba mazito kwake.

Marioo aliendelea kumtambua mwanamitindo huyo kama kipenzi chake.

Kabla ya kudaiwa kuchumbiana na Marioo, Paula alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwimbaji mwingine wa Bongo, Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny. Wawili hao walianza kuchumbiana mwaka wa 2020.

Wakati wa mahojiano, Kajala alifichua kuwa hakufurahi wakati alipogundua  Paula yupo kwenye mahusiano na msanii huyo. Aliweka wazi kuwa pia yeye alikuja kufahamu kuhusu mahusiano hayo kupitia mitandao ya kijamii.

Alifichua kwamba alijaribu sana kumshauri mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 dhidi ya mahusiano na bosi huyo wa Next Level Music lakini juhudi zake  ziliangukia patupu kwani Paula hakusikia.

"Nilijaribu sana kumweleza kwamba hii sio sahihi lakini mtu anaenda anafanya kinyume, inabidi umeacha tu. Ukimwambia asiende na huyo mtu anasema sawa lakini bado anaendelea. Nilijaribu kumzuia sana," alisema.

Aidha, alisema baada ya kushindwa kumshauri Paula dhidi ya uhusiano huo, alimshauri jinsi ya kujiendeleza katika mahusiano.