"Nilishangaa nilipogundua nina ujauzito" Mama Baha afunguka kuhusu kusubiri mtoto miaka mingi

Muhtasari

•Wanjiku alisema aliomba sana na  kusubiri miaka mingi kupata mchumba wa kuanzisha familia naye ila hakuwahi kupoteza matumani.

•Mwigizaji huyo alisema mwanzoni alitilia shaka ujauzito wake na wakati tumbo lake lilipoanza kutokeza ndipo aliamini kuwa kuna kiumbe kilichokuwa kinajiumba ndani yake.

Wanjiku Mburu almaarufu kama Mama Baha
Wanjiku Mburu almaarufu kama Mama Baha
Image: ELIZABETH NGIGI

Mwigizaji Wanjiku Mburu almaarufu kama Mama Baha kutokana na kipindi cha Machachari amekiri kuwa alishangaa sana wakati alipofahamu kuhusu ujauzito wake.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, mwigizaji huyo alisema kuwa hakutarajia angebeba ujauzito kwani tayari  miaka mingi ilikuwa imepita bila yeye kubarikiwa na mtoto.

Wanjiku alisema aliomba sana na  kusubiri miaka mingi kupata mchumba wa kuanzisha familia naye ila hakuwahi kupoteza matumani.

"Mwaka wa 2018  nilienda kuombea maisha yangu. Nilitaka kuombea mwelekeo wa maisha yangu. Kitu kimoja ambacho niliombea ni familia. Baada ya kuomba na kujifunga Mungu aliniahidi kunipa watoto. Nilicheka tu. Niliamua kusubiri. 2018, 2019 hata mtu sikupata sembuse watoto. Niliacha tu" Wanjiku alisema.

Mwigizaji huyo alisema mwanzoni alitilia shaka ujauzito wake na wakati tumbo lake lilipoanza kutokeza ndipo aliamini kuwa kuna kiumbe kilichokuwa kinajiumba ndani yake.

Alisema amekuwa akisubiria sana kuwa mzazi kwa kuwa katika maisha yake yote ameishi kupenda watoto.

"Ni kitu ambacho niliishi kutaka. Hata hivyo nilikuwa nimesema iwapo nitakosa itakuwa sawa tu. Naamini kuwa Mungu hujibu maombi" Wanjiku alisema.

Wanjiku alisema anatarajia kujifungua kati ya mwisho wa mwezi Machi na mwanzoni wa mwezi Aprili.