"Nashangaa watu wa mshahara 20K kwa mwezi mnaishije, ila nawaombea" - Akothee

Akothee alisema yeye gari lake linatumia mafuta elfu 12 kwa siku tatu tu

Muhtasari

• "Siku hizi naingia kwenye duka kuu hata vitu 5 si kiasi chochote chini ya 10k, na nikinunua vya mwezi mzima sio gharama ndogo chini ya 100k" - Akothee

Mwanamuziki na mfanyibiashara Akothee
Mwanamuziki na mfanyibiashara Akothee
Image: Instagram//Akothee

Mwanamuziki na mfanyibiashara Akothee amejipata kwenye midomo ya kejeli baada ya kudai kwamba yeye hajui watu wanaoishi kwa mshahara wa shilingi elfu 20 za Kenya wanamudu maisha aje na huu uchumi ulivyosambaratika vibaya hivi.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Akothee alisema muamini msiamini yeye hajui katu bei ya maziwa au hata sukari.

Mwanamuziki huyo mwenye mikogo kama ya tausi aisema kwamba yeye anachokijua ni kwamba siku hizi anapoelekea kwenye duka la jumla ni kutumia shilingi elfu 10 kwa bidhaa tano tu, na kama ni kuamua kufanya ununuzi wa bidhaa za kumsukuma kwa mwezi basi laki inatoka mfukoni mwake.

“Uwii niamini mimi sijui bei ya maziwa au hata ya sukari, ninachojua siku hizi naingia kwenye duka kuu hata vitu 5 si kiasi chochote chini ya 10k, na nikinunua vya mwezi mzima sio gharama ndogo chini ya 100k kwa vyoo vya vyakula vikavu nk,” alisema Akothee.

Mwanamama huyo pia alizungumzia matumizi ya mafuta kwa gari lake na kusema kwamba kitambo alikuwa anajua akijaza tenki basi inamgharimu shilingi elfu 8 na kutumia mafuta hayo kwa siku nne tu ila siku hizi analazimika kujaza tenki kwa elfu 12 na kumchukua siku tatu pekee.

Kulingana na kulinganisha maisha yake na gharama anazotumia chini ya wiki tu, Akothee alishangaa watu wa mshahara wa elfu 20 wanamudu kivipi maisha kwa mwezi mzima na pesa hizo kidogo kugharimikia mahitaji ya watoto shuleni, chakula na hata kodi ya nyumba wanamoishi. Ila alisema anapofikiria watu kama hao, muda wote anajipata akiwaombea tu kwa Mungu.

“Ninashangaa tu jinsi watu wanaopata 20k kwa mwezi wanaishi na watoto, nyumba za kupanga, bili za hospitali, na maisha ya kila siku. Wee MUNGU AWAONEKANIE WATU WANGU. NAWAOMBEA,” Akothee aling’aka.

Wiki jana mjasiriamali huyo alifichua mipango yake ya mwaka kesho ambapo alisema majaaliwa mwezi Februari atafungua rasmi shule yake ya kuwapa elimu ya bure watoto wa watu wasiojiweza katika jamii kwa kile alikitaja kama ‘angalau elimu ya kujua kuandika na kusoma’ peke yake.