(+video) "Hata mimi huwa naandika nyimbo za mapenzi!" - Reuben Kigame

Alisema wimbo huo aliandikia mkewe takribani miaka 15 iliyopita huku wakijiandaa kusherehekea miaka 15 ya ndoa.

Muhtasari

• Kigame alipuuzilia mbali madai kwamab anaandika nyimbo za mapenzi kutafuta huruma ya wapiga kura na kusema kwamba alianza kuandika ngoma hizo miaka 15 iliyopita.

Mwanasiasa na mtunzi wa muda mrefu wa nyimba za injili za kuabudu Reuben Kigame ameweka wazi kwamba hata yeye ni binadamu na haoni hatia yoyote ya kutunga nyimbo za mapenzi, haswa kwa mkewe kumsifia.

Mwinjilisti huyo ambaye mwaka huu alijitosa katika siasa kuwania nyadhifa ya urais kabla ya tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kumfungia nje aliandika haya kuwajibu wakosoaji waliofokea kwa kupakia wimbo wa mapenzi kwenye mtandao wa YouTube.

Kigame alisema aliandika wimbo huo takribani miaka 15 iliyopita kumsifia mkewe katika mapenzi na si kwamba anaandika kwa kutafuta uungwaji mkono kisiasa.

“Ndiyo, mimi huimba nyimbo za mapenzi pia. Ila ikiwa wakosoaji wangu wanadhani ninafanya hivi kwa sababu ya siasa, niliandika haya kwa ajili ya mke wangu Julie karibu miaka 15 iliyopita. Maisha marefu ya ndoa na familia,” aliandika Kigame kwenye Facebook yake.

“Tangu uje kwangu, nimekuwa mwanaume mwenye furaha. Tangu unipe moyo wako, sijakuwa yule wa awali tena. Maneno hayawezi elezea jinsi gani ninavyokupenda,” baadhi ya beti kwenye wimbo huo zinaimba.

Watu wengi walimsifia kwa kutenga muda wa kutambua mapenzi ya mkewe kwake licha ya kipindi hiki kigumu kilichojawa na misukosuko ya kisiasa haswa anapotumia muda mwingi sana mahakamani kupinga hatua ya IEBC kumfungia nje ya kuwania urais.

“Hii ni nzuri. Inatia moyo kuona kwamba katikati ya shughuli nyingi na machafuko karibu unaweza bado kupata wakati kwa ajili ya watu muhimu zaidi na matukio maalum katika maisha yako. Mungu akubariki kaka,” Clerence Kasyoki aliandika.

“Wow.. Ni vizuri kuwakubali wapendwa wetu... Na kuwathamini pia.. Huenda tusijue tunachothamini mpaka tukipoteze,” mwingine kwa jina Mamake Roy Roy aliandika.

Kigame bado ana Imani kwamba atashiriki katika uchaguzi mkuu licha ya jina lake kutokuwepo katika karatasi za kupiga kura kwa kile alichowashauri wafuasi wake kwamba watumie kalamu na kuandika jina lake chini ya majina matatu ya wagombea urais na kuweka maki kuonesha kwamba wamempigia kura.