Msiwekee tajiri mipaka ya idadi ya wanawake kama mnasema maskini hafai mapenzi - Jimal Rohosafi

Dunia ya sasa mwanaume asiye na mali hadhaminiwi kimapenzi huku wenye nazo wakijilimbikizia makumi ya wanawake.

Muhtasari

• Jimal alionekana kujitetea kwa kuwa na wanawake zaidi ya mmoja baada ya utajiri.

• Alisema kama watu wanadai mwanaume maskini hafai mwanamke basi watu hao hawafai kumwekea tajiri mipaka ya idadi ya wanawake.

Mfanyibiashara huyo amewakashfu wale wanaosema mwanaume maskini hafai kuwa na mpenzi
JIMAL ROHOSAFI Mfanyibiashara huyo amewakashfu wale wanaosema mwanaume maskini hafai kuwa na mpenzi
Image: Instagram

Mfanyibiashara nguli katika sekta ya magari ya uchukuzi wa umma nchini Kenya Jimal Rohosafi ameonekana kujitetea kuhusu kuvurugika kwa mahusiano yake na aliyekuwa mkewe halali Amira baada ya kuanza mahusiano mengine na mwanamitindo Amber Ray.

Katika kile kilichoonekana kama kujitetea kwa kuwa na wanawake zaidi ya mmoja, Jimal ameandika kwenye Instagram yake akiwasuta wale ambao wanajifanya kuwazomea wanaume wenye wanawake wengi kwa kusema kwamba jamii ya aina hiyo haina nafasi kabisa na haifai.

Kulingana na Jimal Rohosafi, jamii ambayo imeweka utabaka kwamba mwanaume asiye na pesa au utajiri hana nafasi ya kutoka kimapenzi na mwanamke yeyote basi jamii hiyo haifai kupewa nafasi hata kidogo kutoa usemi wao kwamba mwanaume mwenye pesa na utajiri hafai kutoka kimapenzi na wanawake zaidi ya mmoja.

Katika utandawazi na usasa wa dunia ya leo, dhana kwamba mwanaume maskini hafai kuwa na mchumba na yule mwenye pesa hafai kutoka na wanawake wengi imekumbatiwa na wengi huku suala hilo sasa likionekana zaidi kuwa kawaida kuliko kuwa ubaguzi wa utabaka.

Jimal amewasuta wale wanaoeneza dhana hiyo na kusema kwamba iwapo wanataka kuikumbatia zaidi basi sharti pia wakubali kwamba mwanaume huyu maskini akija kupata pesa asiwahi kuwekewa mipaka ya idadi ya wanawake atakaotaka kutoka nao.

“Jamii ambayo inamwambia mwanaume aliye maskini hafai mwanamke haina haki ya kumwambia mwanaume ashikamane na mwanamke mmoja anapokuwa Tajiri,” Jimal alirusha kiazi cha moto kwenye ndimi za wenye dhana hiyo.

Wengi wa waliotolea maoni yao kwenye maneno hayo walikuwa wanawake ambao walimkashfu kwa kumwambia kwamba awache kutafuta nukuu za kuhalalisha usaliti katika ndoa kisa mali.

Wiki za hivi karibuni, Jimal ameonekana akimbembeleza mkewe hadharani kwa kumuandikia jumbe za kujuta na kuomba radhi huku akitaka warudiane na kulea wanao kama ilivyokuwa zamani kabla hajapata utajiri na umaarufu ndio aanze kutoka kimapenzi na mwanamitindo Amber Ray.

Amira amefichua juzi kati kwamba amejinunulia gari lake baada ya kudai kwamba Jimal alichukua lile ambao alikuwa amemnunulia kama zawadi enzi za mapenzi yao.