(+video) Nimeacha kutumia bangi, nina saa 48 tangu niache na niko sawa - Tekno Miles

Kwa wale wote mliokuwa mnanikejeli kuwa singeweza kuacha, aibu kwenu, mimi naendelea vizuri - Tekno Miles.

Muhtasari

• Ninapenda jinsi ninavyoendelea nilipata japo kulala kiasi usiku wa jana. Ndio huyu mimi niko vizuri - Tekno alisema.

Msanii kinara wa muziki aina ya Afropop kutoka Nigeria, Tekno Miles amewashangaza wengi baada ya kudokeza kwamba ameamua kuacha kabisa matumizi ya bangi au marijuana kwa jina lingine.

Kupitia video ambapo msanii huyo alipakia kwenye instastories zake, alidokeza kuwa alifikia uamuzi huo na mpaka Alhmamisi tayari alikuwa amemaliza zaidi ya saa 48 sawa na siku mbili bila kutumia kileo hicho.

Miles alisema kuwa awali hangeweza kukaa bila kutumia bangi hata usiku mmoja lakini sasa hata yeye haamini kama kweli ameweza kukaa zaidi ya masaa 48 pasi na kukaribia bangi.

“Huyu ni mimi, saa 48 baadae au tuseme zaidi ya saa hizo, bila bangi, bila marijuana, ninapenda jinsi ninavyoendelea nilipata japo kulala kiasi usiku wa jana. Ndio huyu mimi niko vizuri, macho yangu sasa yako vizuri hayana zile dalili za kuonesha utumizi wa vileo. Najua itakuwa vizuri hata zaidi,” Tekno alisema.

Vile vile aliwasuta vikali wale waliojaribu kumkejeli kuwa hangeweza kuachana na uraibu ho na kusema kwamba watashangaa sana baada ya siku thelathini atakaporudi kutoa ushuhuda wake jinsi amekuwa akihisi bila vileo.

“Kwa wale wote mliokuwa mnanikejeli kuwa singeweza kuacha, aibu kwenu, mimi naendelea vizuri,” Tekno alisema kwenye instastory yake.

Tekno aiweka wazi kwamba kwa muda mrefu amekuwa akiteseka kutokana na uraibu wa matumizi ya bangi ila sasa ndio kama mwanzo mkoko unaalika maua katika maisha yake kwa kuachana kabisa na marijuana.

Tekno si msanii wa kwanza kuweka wazi kuwa amekuwa akitumia dawa za kulevya ili kumpa mihemko ya kutimba studioni na kufanya ngoma ambazo aghalabu huwa na mapokezi makubwa kwa mashabiki wake.

Mkali huyo kwa sasa anazidi kutamba kwa kibao chake kipya cha After Party baada ya kuvuma na collabo aliyoshirikishwa na Kizz Daniel kwa jina Buga.