Ahsante kwa kuendelea kunipenda na wanangu - Diana amwambia Bahati

Marua alisema kuwa anajihisi mwenye faraja kubwa kuitwa mama na watoto wanne katika familia yake.

Muhtasari

• Marua anamsifia Bahati kwa mapenzi yasiyo ya ukomo haswa baada ya wanamitandao kumwekea shinikizo la kumuacha kutokana ufichuzi kwenye video yake.

Diana amshukuru Bahati kwa kuendelea kumpenda licha ya mapungufu yake
Diana amshukuru Bahati kwa kuendelea kumpenda licha ya mapungufu yake
Image: Instagram

Mwanablogu wa YouTube Diana Marua amempongeza mumewe Bahati kwa kumpenda bila kikomo wala kipimo hata baada ya kufichua maisha yake ya awali jinsi yalivyokuwa yamekumbwa na ukungu mkubwa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diana Marua alipakia msururu wa picha zake na Bahati pamoja na watoto wao wote familia nzima na kusema kwamba bila familia hiyo bila shaka angejihisi mpweke sana.

“Mpenzi wangu @BahatiKenya asante kwa Kutupenda kupita kawaida. Tunakuthamini,” Marua alimwambia Bahati.

Kando na hayo, pia Marua alisema anajihisi kubarikiwa kuitwa mama na watoto wane, wakiwemo watatu wa kuwazaa na mmoja wa kumuasili ambaye ni Morgan.

Aliwamiminia sifa watoto hao kwa kuleta furaha na joto katika nyumba yao na maisha kwa ujumla na kusema kwamba kuwa mama ndio uamuzi bora zaidi ambao aliuchukua pasi na kujuta.

“Zawadi kubwa kuliko zote... Zawadi ya kuitwa Mummy ️ @Morgan_Bahati @HeavenBahati @MajestyBahati na @Malaika_Bahati asante kwa Kuleta utimilifu mkubwa maishani mwangu,” Marua alisema.

Kumshukuru kwake mumewe Bahati kunajiri wakati ambapo mawimbi ya kila aina yanailenga ndoa yao haswa baada ya watumizi wa mitandao ya kijamii kuibua video aliyoipakia kwenye YouTube miaka miwili iliyopita akieleza jinsi alikuwa anachepuka na wanaume kadhaa kwa ajili ya matunzo na mahitaji mengine ya kimaisha.

Bahati muda wote amekuwa akisimama upande wa familia yake na hata Kumtetea dhidi ya masimango na matusi ambayo amekuwa akirushiwa haswa baada ya ufichuzi wa ukweli kuhusu maisha yake ya awali kabla ndoa.