Asia Brown kuanza shule Januari 2023 - Vera Sidika afichua

Ni mtoto mwerevu tena mwenye akili kwa taarifa yenu,” Sidika alijigamba.

Muhtasari

• Anaanza shule Januari, nina Imani atafurahia sana kwa sababu anapenda watoto - Sidika.

Sidika adokeza bei ya nguo ya mwanawe Asia Brown
Sidika adokeza bei ya nguo ya mwanawe Asia Brown
Image: Instagram

Mwanasosholaiti Vera Sidika amefichua kuwa binti yake sasa ni mtu mzima na Januari mwakani atajiunga na shule ya chekechea.

Sidika alikuwa akijibu maswali ya mashabiki wake kupitia kipindi cha Instagram cha maswali na majibu ambapo wengi walitaka kuona jinsi mtoto wao amekua. Tangu wamsherehekee kufikisha mwaka mmoja, Sidika amekuwa mchache wa kuchapisha picha na video za mwanawe na hivyo kuwakosesha raha mashabiki wake ambao walikuwa wameanza kupenda hatua za mtoto Asia Brown

“Asia ni mtu mzima sasa amekua. Anakimbia kote akisambaratisha kila kitu. Msichana hata hawezi kutulia kwa dakika, kumbadilisha nepi ni kibarua kigumu hata yaya anambadilisha kama amesimama ama akiendelea kutembea. Anaanza shule Januari, nina Imani atafurahia sana kwa sababu anapenda watoto. Uso wake unawake kila anapokuwa na watoto wengine hata kama ni kucheza nao siku nzima hicho ndicho anakipenda. Ni mtoto mwerevu tena mwenye akili kwa taarifa yenu,” Sidika alijigamba.

Pia alisema kuwa mtoto huyo alianza kuzungumza kitambo na kukimbia nyumba nzima akiwashrutisha kitu cha kumfanyia.

“Ndio, alianza kuzungumza kitambo, alisema baba kwanza na hilo ndilo neno ambalo anasema muda wote. Hata nikimwambia aseme mama, anasema baba makusudi,” alisema.

Mwanasosholaiti huyo pia alipuuzilia mbali madai ya hivi karibuni kwamba yu mjamzito kwa mtoto mwingine.

Alisema kuwa hiyo video na picha ambazo zimekuwa zikisambazwa ni zile ambazo alichukua kipindi akitangaza ujauzito wake na mchumba wake Brown Mauzo.