Sarah Michelloti amchekelea Harmonize baada ya kuachwa na Kajala

Michelloti waliachana na Harmonize miezi michache baada ya kuondoka WCB Wasafi.

Muhtasari

• Vyanzo vya habari vinadai Michelloti alikuwa mwezeshaji mkubwa wa Harmonize kipindi anaondoka WCB Wasafi.

Michelloti amtuoia kejeli Harmonize
Michelloti amtuoia kejeli Harmonize
Image: Instagram

Aliyekuwa mpenzi wa Harmonize, mwanamitindo Sarah Michelloti kutoka Italia amevunja ukimya wake kuhusu sakata la kutengana kwa Harmonize na mwigizaji Kajala Frida Masanja.

Michelloti kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliandika ujumbe uliolenga kumfuma kifuani moja kwa moja Harmonize huku akionekana kumkejeli kuwa alimuacha akifikiria anakokimbilia amepata mapenzi ya kweli kumbe huko ndiko kutendwa vibaya hata zaidi.

Alisema njia pekee na ya hakika katika maisha kufanikisha furaha yako ni kupenda mtu ambaye pia anakupenda, lakini kwa Harmonize, alimpenda Kajala ambaye alikuwa analenga mafanikio yake ya kimuziki – baada ya kupata magari ya kifahari kama zawadi ameamua kumbwaga na kumuacha maskini wa watu hoi bin taaban katikati ya barabara.

“Kuna njia moja tu ya kupata furaha katika maisha haya, kupenda na kupendwa,” Michelloti alichokoza.

Kajala ambaye pia alikuwa meneja wa Harmonize alimwacha mapema mwezi huu kwa madai ya kumpa ujauzito mwanamke mwingine mdogo.

Kajala alisema aliifedhehesha familia yake na marafiki zake kwa kumrudisha lakini hatarudia kosa hilo.

Kajala pia ameshusha picha zote alizowahi kupiga na Harmonize. Katika ukurasa wake wa Instagram ambapo Kajala alimtoa hadharani mwanamuziki huyo aliandika,

“Mimi ni mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na pia kusamehe, lakini kwa hili nataka kuchekwa, kukosolewa na hata kubezwa.”

Michelloti miezi michache iliyopita alizua timbwiri baada ya kuelekea mahakamani kudai haki na sehemu ya mali ya Harmonize kwa kile kilisemekana kuwa ndiye alikuwa mwezeshaji mkubwa wa msanii huyo wakati aliondoka Wasafi na kuanza kujitegemea.