Dadake Akothee, Cebbie Koks afunga harusi ya kitamaduni na mchumba Steve Ogolla

Cebbie na dadake mkubwa Akothee hawajakuwa na maelewano mazuri na haijulikani iwapo Akothee alihudhuria harusi hiyo iliyofanyika Nyanza.

Muhtasari

• Watu maarufu akiwemo mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o alihudhuria hafla hiyo ya kitamaduni.

Cebbie Koks wakicheza densi na mpenziwe Steve Ogolla
Cebbie Koks wakicheza densi na mpenziwe Steve Ogolla
Image: Tiktok

Dadake mwanamuziki na mjasiriamali Akothee, Cebbie Koks hatimaye amefunga harusi ya kitamaduni na mpenzi wake wa muda mrefu, mwanasheria Steve Ogolla.

Katika picha ambazo zilisambazwa mitandaoni Jumatano Desemba 28, wawili hao walifanya harusi ya kitamaduni katika moja ya mandhari safi eneo la Nyanza ambapo watu wengi maarufu walihudhuria  hafla hiyo inayompendeza Mungu.

Katika siku yake maalum, Cebbie alivaa vazi la kupendeza la rangi nyeupe na dhahabu, huku Steve Ogolla akiwa amevalia mavazi meupe, kofia ya kijani na fimbo, kwa muonekano wa Wanaigeria.

Mwanasheria Steve Ogolla alimchumbia Cebbie Koks hivi majuzi katika sherehe nzuri katika ukumbi uliopambwa kwa umaridadi ambapo alipiga magoti chini kiungwana na kumvisha pete ya uchumba.

Alimzawadia maua huku wakitembea pamoja hadi kwenye seti iliyokuwa na maneno 'Marry Me' kwa rangi nyeupe. Baadae kwenye ukurasa wake wa Facebook, Ogolla aliandika kwa furaha akisema kuwa hatimaye mpenzi wake Koks alikubali ombi lake la ndoa.

Wafuasi kwenye mitandao ya kijamii wamewatumia wanandoa hao salamu za pongezi, wakiwatakia heri katika umoja wao.

Haijajulikana wazi iwapo dadake Cebbie, Akothee alihudhuria hafla hiyo, lakini inaeleweka kuwa Akothee hivi majuzi aliharibikiwa na ujauzito wake.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na maneno mitandaoni kuwa Akothee na dada zake hawana maelewano mazuri katika kile amekuwa akitaja kuwa ni dada zake wadogo kuonea gere mafanikio yake.

Licha ya kuwepo kwa tofauti kubwa baina ya Akothee na wadogo zake, watu walipomshambulia Koks kwenye mitandao ya kijamii baada ya kukubali uchumba na Ogolla, mama huyo wa watoto watano alimtetea vikali huku akiwakashfu wote haswa blogu ambazo zimekuwa zikiandika mabaya pekee kuhusu familia yao.