Sallam SK: Mimi sina urafiki na Harmonize, alinisalimia tu ili kutafuta kiki kwa jina langu

Meneja huyo wa Diamond alionekana wiki chache zilizopita akisalimiana na Harmonize na kuzua gumzo kuwa huenda ameondoka WCB.

Muhtasari

• Sallam alisema Harmonize alirudia kumsalimia mara mbili baada ya kutga kamera ili kupata kiki kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo alilifanikisha.

Sallam SK amjibu Harmonize
Sallam SK amjibu Harmonize
Image: Instagram

Baada ya kuhusishwa na hadithi tofuati katika siku za hivi karibuni kuhusu kutaka kuondoka Wasafi na kufanya kazi na Harmonize, meneja wa Diamond Sallam SK Mendez kwa mara ya kwanza amevunja ukimya.

Wiki kadhaa zilizopita, Sallam SK ambaye ni meneja mkuu wa bosi wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz alionekana kwenye video na picha akiwa anasalimiana na Harmonize – msanii ambaye ni hasimu mkuu wa kimuziki kwa Diamond.

Katika mahojiano na kituo cha habari cha Wasafi, Sallam SK alikanusha ripoti zilizopo mitandaoni kuwa anataka kuondoka Wasafi na kuanza kufanya kazi na Konde Gang ya Harmonize.

 Alisema kuwa yeye alikuwa zake wakati Harmonize alipomfuata na kumsalimia kawaida tu kabla ya kupita. Sallam alisema kuwa Harmonize alirudi tena na kumsalimia kwa mara ya pili katika kile alisema “alikuwa anatafuta kiki na alikuwa ametega kamera zake kuchukua tukio hilo.”

Sallam alisema msanii huyo ambaye zamani alikuwa katika lebo ya Wasafi alimfuata mwanafamilia mmoja wa Sallam mkoani Morogoro ambapo alimuelezea nia yake ya kutaka kuzika uhasama wake na Sallam.

“Kwa hivyo video hiyo ambayo imesambaa mitandaoni ilikuwa mara ya pili alipokuwa akiniamkia. Alipita kwanza na kunisalimia nafikiri kwa salamu ya pili, alikuwa anatafuta maudhui kwani alikuwa ameweka kamera zake,” Sallam alisema huku akitetea hatua yake ya kuhudhuria tamasha ambalo Harmonize alikuwa anatumbuiza Zanzibar kwa kusema kuwa “Nilikuwa ninajuana na meneja wa eneo lile na nilienda kujistarehesha tu.”

Meneja huyo alimkanyagia Harmonize chini kwa kusema kuwa ije mvua liwake jua, katu hawezi kufanya kazi naye kama meneja kwa kuwa yeye ana ukubuhu mwingi katika taaluma ya muziki.

Alisema kuwa njia pekee ya kufanya kazi na Harmonize si kuwa meneja wake bali ni endapo atafungua lebo yake na kumpa mkataba kama msanii chini yake.