Wema Sepetu afunguka alivyotongozwa na Whozu, Christina Shusho ajitolea kuongoza harusi yao

Alisema baada ya kukutana 2019 walianza urafiki kabla ya kujitosa kwenye mahusiano 2022.

Muhtasari

•Christina Shusho alionekana kupendezwa sana na mahaba kati ya wawili hao na hata akijitolea kuongoza ndoa yao.

•Sepetu amesema mahusiano ya awali ya Whozuu tayari yalikuwa yamesambaratika wakati walipoanza kuchumbiana.

Image: INSTAGRAM// WHOZU

Siku ya Jumatano, muigizaji wa Bongo Wema Sepetu aliwakaribisha wageni kadhaa nyumbani kwake kwa kikao cha Iftar.

Sepetu alikuwa amevalia gauni zuri la Kiislamu huku mchumba wake Whozu akiwa amevalia kanzu nyeupe na baada ya picha zao kusambaa mitandaoni kukaibuka madai kuwa walikuwa wanafunga pingu za maisha.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz alichapisha video yake nzuri na   Whozu wakiwa wamevalia mavazi hayo yaliyofanana huku wakikumbatiana kimahaba na kubusu midomoni.

"Kwani nikiwa speechless kuna tatizo," aliandika chini ya video hiyo ambayo alichapisha kwenye Instagram.

Mamia ya wanamitandao walifurika kwenye sehemu ya maoni ya chapisho hilo na kuwaandikia wapenzi hao jumbe maalum.

Mwimbaji Christina Shusho alionekana kupendezwa sana na mahaba kati ya wawili hao na hata akijitolea kuongoza ndoa yao.

"Mchungaji wa kufungisha ndoa niko hapa jamani @Whozu unakwama wapi mpendwa. Mbona chap tu," alijibu Shusho.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Iftar, Sepetu hata hivyo aliweka wazi kuwa alivalia vizuri kwa hafla hiyo ya Kiislamu.

Wakati huo, muigizaji huyo alifunguka jinsi alivyokutana na Whozu na hatimaye kuanza kuchumbiana mwaka jana.

"Tulikuwa Dodoma, nilikuwa nimeenda kwa ajili ya kazi. Yeye alikuwa amefika kwa ajili ya masuala yake mwenyewe," alisema.

Alisema baada ya kukutana mwaka wa 2019 walishiriki uhusiano wa kirafiki kabla ya kujitosa kwenye mahusiano mwaka jana.

"Tumekuwa marafiki. Wakati mwingine nilikuwa namshauri kwenye mambo yake ya mapenzi. Tulianza kuchumbiana mwezi wa nne mwaka jana," alisema

Mwimbaji Whozu alikuwa kwenye mahusiano mengine wakati alipokutana na muigizaji huyo na kuanza urafiki.

Sepetu hata hivyo ameeleza kuwa mahusiano ya awali ya mchumba huyo wake tayari yalikuwa yamefika kikomo walipoanza uchumba.

"Alikuwa na shida zake yeye na mtu wake. Mimi sikutaka kuingilia. Nilikuwa wa msaada kwa namna moja ama nyingine pale ambapo alihitaji sapoti. Tulikuwa naye kama rafiki kwa miaka miwili. Niseme nini, jambo moja lilipelekea jingine.. sijawahi kuvuruga mahusiano ya watu. Tukianza mahusiano alikuwa single sana. Alikuwa bila mchumba kwa takriban miezi mitano," alisema muigizaji huyo.

Wawili hao waliweka mahusiano yao wazi mwaka jana wakati mpenzi huyo wa zamani wa Diamond akiadhimisha siku ya kuzaliwa.