Rayvanny na wimbo kumhongera mjamzito baada ya Ex wake Paula kuonesha ujauzito wa Marioo

"Nikiona tumbo lako, tabasamu lako kweli kitanda hakiongopei, nasubiri siku yako uzae baby wako zawadi kemkem tukugee...nikiona pua yako domo macho yako hakuna haja ya DNA." aliimba Rayvanny.

Muhtasari

• Itakumbukwa Rayvanny alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na binti Paula kwa miezi kadhaa baada ya kumtema mpenzi wake wa kwanza ambaye wana mtoto mmoja pamoja.

• Hata hivyo, unaambiwa mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani! Rayvanny alijirudi kwa hisia zake kwa mama mtoto wake Fahyvanny na kurudiana naye huku akimuacha Paula kwenye mataa.

Rayvanny awatolea wimbo wa pongezi Marioo na Paula
Rayvanny awatolea wimbo wa pongezi Marioo na Paula
Image: Instagram

Siku chache baada ya binti wa mwigizaji mkongwe wa filamu za Bongo, Fridah Kajala, Paula kutangaza kuwa anatarajia mtoto pamoja na mpenzi wake Marioo, mpenzi wake wa zamani Rayvanny ameingia studioni na kuwatungia wimbo wa hongera.

Rayvanny ambaye ni mpenzi wa zamani wa Paula aliachia wimbo huo kwa jina ‘Hongera’ mapema Jumapili asubuhi ukiwa umebeba ujumbe wa kumhongera mwanamke mjamzito.

Japo hakutaja moja kwa moja jina la Paula kwenye utunzi wake, wengi wanahisi ujumbe katika wimbo huo unaelekezwa kwa wapenzi wapya, Marioo na Paula ambao wametangaza kutarajia mwanao hivi karibuni.

“Hongera unaitwa mama, unaitwa mama leo, ni furaha pande zote, sio tu kwa babu, bibi, baba au mama. Imekuja Baraka kwenu, Mungu amemleta mwana, Te amo tanto [nakupenda sana], wewe na yeye mnaendana, mpate katoto half-cast, kawaite mama na baba…” sehemu ya mistari kwenye wimbo iliimba.

“…nikiona tumbo lako, tabasamu lako kweli kitanda hakiongopei, nasubiri siku yako uzae baby wako zawadi kemkem tukugee. Uzuri wa sura yako na mtoto wako kweli damu haiongopei, nikiona pua yako domo macho yako hakuna haja ya DNA, hongera unaitwa mama, unaitwa mama…” Rayvanny aliimba Zaidi.

Itakumbukwa Rayvanny alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na binti Paula kwa miezi kadhaa baada ya kumtema mpenzi wake wa kwanza ambaye wana mtoto mmoja pamoja.

Hata hivyo, unaambiwa mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani! Rayvanny alijirudi kwa hisia zake kwa mama mtoto wake Fahyvanny na kurudiana naye huku akimuacha Paula kwenye mataa.

Msanii mwenza, Marioo alitumia fursa hiyo na kumchukua Paula na kumpa faraja kwenye kifua chake mwaka jana, miezi kadhaa baadae hivi majuzi walitangaza kutarajia mtoto wao wa kwanza wakiambataniza tangazo hilo na picha za ujauzito.

Hii ilikuja kama mshangao kwa watu ambao walikuwa wanadhani wawili hao walikuwa wanatania kuwa katika mahusiano, haswa baada ya Paula kuchambana na Rayvanny vikali wakati alikuwa anazungumzia maisha yake pamoja na mama yake Kajala kwenye moja ya kipindi cha uhalisia runingani kwa jina ‘Behind the Gram’.

Paula pia alidai kulipiwa mahari ya shilingi milioni 100 za kitanzania na Marioo, wakati alikuwa anajibu swali kutoka kwa mwandishi mmoja wa habari za burudani.