Manzi wa Meru: Mimi na mpenzi wangu tunatarajia mtoto kupitia surrogacy, mimba iko miezi 2!

Jude Magambo na mpenzi wake Ray - wote wanaume - alisema walitafuta mrembo wa kuwabebea ujauzito na kumlipa pesa nyingi kabla ya kukubali kuchangia mbegu ya kike na kuthibitisha mtoto atakuwa na wazazi 3.

Muhtasari

• “Tulichangia mbegu sisi sote watatu, mtoto atakuwa wetu – mimi na Ray na huyo mrembo, hiyo ndoto ni mtoto wa watu 3. Hatatoka akifanana mtu yeyote, atatufanana sisi wote watatu.”

Jude Magambo wanatarajia mtoto
Jude Magambo wanatarajia mtoto
Image: TikTok, screengrab

Mwanachama wa LGBTQ, Jude Magambo maarufu kama Manzi wa Meru amethibitisha kwamba yeye na mpenzi wake – wote wanaume – wanatarajia mtoto.

Akizungumza na KOM, Magambo ambaye wamechumbiana na mpenzi wake kwa miezi sita alithibitisha kwamba walifanikisha hatua hiyo kwa kumtafuta mrembo ambaye alikuwa tayari kuwabebea ujauzito kwa njia ya ‘surrogacy’ kwa kimombo.

“Ray ni mmoja wa watu ambao nimechumbiana naye kwa muda mrefu kiasi, sababu mimi sijawahi chumbiana na mtu Zaidi ya miezi 2, lakini Ray tumechumbiana kwa miezi 6 sasa. Kwa hiyo tumeenda mpaka kufikia hatua ya kufanya surrogacy na tayari ilishafanyika, tulimlipa pesa nyingi mrembo wa kutubebea ujauzito. Kwa sasa anabeba mimba yetu na nina furaha sana,” Manzi wa Meru alisema.

Alipoulizwa kama anaweza dokeza utambulisho wa huyo mrembo anayebeba mimba yao, Manzi wa Meru alisema kwamba mrembo huyo anapenda usiri wake na wala hakati picha, lakini akathibitisha kwamba ujauzito tayari umeshatimia miezi miwili.

“Ni mtu ambaye hapendi picha kabisa, hataki kuonekana lakini kila kitu kwa sasa kiko sawa na mtoto wetu yuko njiani atakuja hivi karibuni, na nina furaha ghaya. Nafikiri kwa sasa mimba ni ya miezi 2,” Magambo alisema.

 Hata hivyo, katika taratibu za surrogacy, inafahamika kwamba mwanamke na mwanamume wote wanajitolea kutoa mbegu zao kabla ya kuwekwa kwa mwili wa mwanamke mwingine ambaye anailea mimba hiyo kwa kimombo ‘surrogate mother’.

Lakini kwa hawa mawili, Jude na Ray, wote ni wanaume, kwa hiyo iliwezekanaje kufanikisha mimba wakati mbegu ya kike hawana?

Jude anafafanua;

“Tulichangia mbegu sisi sote watatu, mtoto atakuwa wetu – mimi na Ray na huyo mrembo, hiyo ndoto ni mtoto wa watu 3. Hatatoka akifanana mtu yeyote, atatufanana sisi wote watatu.”

Kuhusu gharama za kufanikisha mchakato huo, Manzi wa Meru alikiri kwamba ni mchakato ghali sana lakini akasema yeye ni mtu ambaye anapata ufadhili kifedha kutoka sehemu mbali mbali duniani, ikiwemo Marekani na mataifa mengine.

“Surogacy ni mchakato ghali lakini unajua mimi nina mashabiki wengi kutoka Marekani, nina watu wanaonipa msaada kifedha kwa hiyo haikunikalia ngumu. Pindi nilipowaambia kwamba nataka kufanya hivi waliniuliza tu kiasi cha pesa ninahitaji na dakika mbili nikawatumia maelezo yangu ya benki na hivyo nikapata pesa,” alieleza.