Diamond Platnumz avunja rekodi ya Afrika Kusini mwa Sahara

Video zake zimetazamwa mara 2.0003B kwenye Youtube.

Muhtasari

•Diamond ameibuka kuwa msanii wa kwanza kutoka  Kusini mwa Jangwa la Sahara kufikisha views bilioni mbili kwenye mtandao wa YouTube.

•Kando na muziki, staa huyo wa Bongo pia ametajwa miongoni mwa wanamuziki tajiri zaidi barani Afrika.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz ameweka rekodi mpya kwenye jukwaa la kimataifa la video la Youtube.

Diamond ameibuka kuwa msanii wa kwanza kutoka  Kusini mwa Jangwa la Sahara kufikisha views bilioni mbili kwenye mtandao wa YouTube.

Kufikia Alhamisi, Disemba 15, video za mwimbaji huyo zilikuwa zimetazamwa mara 2.0003B kwenye mtandao huo.

"Diamond Platnumz amepitisha jumla ya views bilioni mbili kwenye YouTube. Yeye ndiye msanii wa kwanza wa Kusini mwa Sahara kufikisha hatua hii," lebo ya Diamond WCB ilisherehekea kupitia mtandao wa Instagram.

Bosi huyo wa WCB ameorodheshwa miongoni mwa wasanii bora wa bara Afrika kwa kuzingatia talanta, mafanikio na hata utajiri.

Wengine kwenye orodha hiyo ni pamoja na Burna Boy, Davido, Wiz Kid, Fally Ipupa miongoni mwa wasanii wengine.

Kando na muziki, staa huyo wa Bongo pia ametajwa miongoni mwa wanamuziki tajiri zaidi barani Afrika.

Mwaka jana Diamond alikosoa orodha ya Forbes iliyowaonesha wanamuziki tajiri wa Afrika na kumuweka katika nafasi ya 20.

’Wakati mwengine nitafuteni katika Google ili kujua thamani yangu’’, Diamond aliandika katika ukurasa wake wa Instagram ‘’kabla ya kuniweka katika orodha yenu ya matajiri !"

Mwaka wa 2020 mwimbaji huyo kutoka Tanzania aliibuka kuwa mwanamuziki wa kwanza katika jangwa la Sahara kufikisha watazamaji bilioni moja kwenye mtandao wa YouTube.

Kwenye mtandao wa Instagram, staa huyo wa Bongo kwa sasa ana wafuasi milioni 15.5 huku akiwa anafuatilia akaunti  1330 pekee.

Diamond pia anafuatiliwa na watu milioni 6.8 kwenye Facebook na wengine milioni 1.2 kwenye mtandao wa Twitter.