"Ogopa Nairobi!" Gidi awasihi wakazi wa Nairobi kutumia mipira kufuatia mlipuko wa kisonono

Gidi aliwataka watu wanaopanga kushiriki tendo la ndoa wikendi hii kuzingatia kutumia kinga.

Muhtasari

•Gidi sasa amewaonya watu ambao wanaishi katika jiji la Nairobi kuwa waangalifu zaidi tunapoingia wikendi.

•"Kama ni lazima ufanye ngono, hakikisha umetumia mpira tafadhali. Jikinge. Hii ni Kanairo, Nairobi," alisema.

Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji mahiri wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo Gidi Ogidi amewatahahadharisha Wakenya hasa katika kaunti ya Nairobi kuhusu ugonjwa hatari wa zinaa wa kisonono.

Hii inafuatia ripoti za hivi majuzi za kuzuka kwa aina sugu ya ugonjwa wa kisonono katika mji huo mkuu wa Kenya.

Gidi sasa amewaonya watu ambao wanaishi katika jiji la Nairobi kuwa waangalifu zaidi tunapoingia wikendi.

"Ogopa sana Nairobi, jikinge kutokana na ugonjwa wa kisonono," mtangazaji huyo alisema siku ya Ijumaa.

Gidi aliwataka watu ambao wanapanga kushiriki tendo la ndoa wikendi hii inayokuja kuzingatia kutumia kinga.

"Kama ni lazima ufanye ngono, hakikisha umetumia mpira tafadhali. Jikinge. Hii ni Kanairo, Nairobi," alisema.

Siku ya Jumatano, Januari 12, gazeti la The Star liliripoti kwamba ugonjwa wa kisonono ambao unastahimili dawa nyingi zinazotumiwa kutibu ugonjwa huo wa zinaa sasa uko jijini Nairobi.

Ugunduzi huo, ulioelezewa na wataalamu wa afya kuwa "wa wasiwasi", unamaanisha kuwa Wakenya wengi wana maambukizi ambayo karibu hayatibiki ambayo yanaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa kudumu kwa mfumo wa uzazi.

Ugonjwa wa kisonono unaostahimili dawa ulitengwa kutoka kwa sampuli iliyochukuliwa kutoka kwa mmoja wa wafanyabiashara ya ngono 24 wagonjwa kutoka Nairobi mwaka jana.

Amina Abdullahi, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Madaktari ya Kenya (Kemri) ambaye aligundua ugunduzi huo, alisema wanawake wengi wagonjwa hawakuwa hata na dalili za kiafya za kisonono.

"Matokeo yalionyesha upinzani kamili (asilimia 100) kwa dawa zote za kuua viini," aliripoti.

Dawa ambazo hazikufaulu ni pamoja na ciprofloxacin na ceftriaxone, ambazo ziko katika kanuni ya sasa ya matibabu ya magonjwa ya zinaa nchini Kenya.

"Matokeo kutoka kwa utafiti huu yanaonyesha uwezekano wa kisonono sugu kwa dawa nyingi kusambaa miongoni mwa wafanyabiashara ya ngono wa kike jijini Nairobi, jambo ambalo linatia wasiwasi," alisema.

Kisonono huathiri wanaume na wanawake na kwa kawaida huenezwa kwa njia ya ngono ua mdomo, makalio au uke. Maambukizi mara chache hutoa dalili zinazoonekana.

Hata hivyo, dalili zinaweza kujumuisha kutokwa na maji, kuungua wakati wa kukojoa, vidonda visivyo vya kawaida au upele.