"Tunakula sumu!" Mwanamke asikitika baada ya kuuziwa avocado zilizopakwa rangi kuonekana zimekomaa Murang’a (+video)

“Shida ni kwamba, hata hatujui ni kitu gani kimepakwa kwenye maparachichi haya. Tutakula mavi, tunakula sumu," Mwanamke huyo alilalamika.

Muhtasari

•Mwanamke huyo alionekana akifuta rangi nyeusi iliyopakwa kwenye maparachichi na kulalamika kwamba hajui ni nini hasa kilikuwa kimepakwa kwenye matunda hayo matamu.

•Mlalamishi alidai kuwa wafanyabiashara wanatumia mbinu hiyo kuuza matunda yao haraka sana kwa watu wanaotumia barabara ya Murang’a-Nairobi.

Image: HISANI

Mwanamke mmoja Mkenya ameibua malalamishi mitandaoni baada ya kununua matunda ya parachichi yaliyokuwa yamepakwa rangi rangi nyeusi ili yaonekane kama kwamba yamekomaa.

Katika video ambayo imekuwa ikivuma kwenye mitandao ya kijamii, mwanamke huyo ambaye hajatambulika anaonekana akifuta rangi nyeusi iliyopakwa kwenye maparachichi na kulalamika kwamba hajui ni nini hasa kilikuwa kimepakwa kwenye matunda hayo matamu.

Alifichua kuwa baada ya kuyaweka kwa muda ili kuiva, maparachichi hayo hayakuwa yakiiva bali yalikuwa yakioza.

“Angalia nini kinafanyika kwa maparachichi haya. Kwanza utaona ni parachichi la purple kwa sababu ni Hass. Nilinunua yangu wiki moja nikaweka yaive, kukuja kuangalia nikapata hayaivi lakini sasa nimeshtuka. Kuenda kutoa maparachichi yangu yenye yananikalia kama yameiva, unaenda unapata si kuiva imeiva ni kuoza,” alisikika mwanamke huyo akilalamika kwenye video hiyo.

Mwanamke huyo alifichua kuwa alinunua maparachichi yenye sura nzuri katika eneo la Kaharati, kaunti ya Murang’a bila kujua kwamba yalikuwa yamepakwa rangi ili yaonekane ya kuvutia.

“Mimi niliona maparachichi yameiva vizuri, ya rangi ya zambarau, makubwa, hass nikasema haya siachi. Wadau kuja kuangalia nikapata maparachichi yamepakwa rangi. Ukienda kupanguza utapata yanaonekana meusi mwanzoni lakini yanakuwa kijani kibichi baada ya kupangusa,” alisema.

Alidai kuwa wafanyabiashara wanatumia mbinu hiyo kuuza matunda yao haraka sana kwa watu wanaotumia barabara ya Murang’a-Nairobi.

“Sijui hii ni rangi gani. Shida ni kwamba, hata hatujui ni kitu gani ambacho kimepakwa kwenye maparachichi haya. Tutakula mavi, tunakula sumu,” alilalamika.

Aliendelea kuonya watu dhidi ya kununua parachichi kando ya barabara ya Murang’a-Nairobi akisema kwamba wanaweza kuishia kulaghaiwa kama yeye.

“Hii ni sumu, sijui tunakoelekea kama Wakenya. Angalieni tamaa ya pesa, hivi ndivyo nilivyokuja kuona. Maparachichi yangu hayaivi, yanaoza. Unajiuliza ni rangi gani hii ambayo wameweka kwenye parachichi hizi,” mwanamke huyo alisema kabla ya kwenda kutupa matunda yaliyooza kwenye pipa la vumbi.

Mwanamke huyo alisema kuwa alichagua kutupa maparachichi hayo kwa kuwa aliogopa kula kitu ambacho hana uhakika kama kina sumu.