Waliokuwa wapenzi wa Diamond, Wema Sepetu na Hamisa Mobetto wazungumzia ugomvi

"Napenda kuacha mambo yaliyopita yapite. Huwa sipendi sana kushikilia ugomvi," Wema Sepetu alisema.

Muhtasari

•Muigizaji Wema Sepetu alifutilia mbali tetesi za mitandaoni kwamba amewahi kuwa na ugomvi na Hamisa Mobetto.

•Mobetto alifichua Sepetu amekuwa rafiki mzuri kwake kwa muda mrefu na alimsaidia kukuza kazi na umaarufu wake.

•Wawili hao wamewahi kuchumbiana na staa wa Bongo Diamond Platnumz katika nyakati tofauti.

Hamisa Mobetto na Wema Sepetu
Image: HISANI// HAMISA MOBETTO

Siku ya Jumatano, muigizaji maarufu wa Bongo Wema Sepetu alimkaribisha mwanamitindo Hamisa Mobetto miongoni mwa wageni wengine kadhaa nyumbani kwake kwa ajili ya sherehe za Iftar.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla hiyo, Sepetu alizungumzia uhusiano wake na mwanamitindo huyo.

Ni wakati huo ambapo alifutilia mbali tetesi za mitandaoni kwamba amewahi kuwa na ugomvi na Mobetto.

"Hatujawahi kugombana mimi na Hamisa. Yeye ni kipenzi changu kila siku," alisema.

Mpenzi huyo wa mwimbaji Whozu aliweka wazi kuwa yeye na Mobetto wamekuwa marafiki wa karibu kwa miaka mingi.

Alisema alipata kujuana na mama huyo wa watoto wawili miaka mingi iliyopita kabla hata hajapata umaarufu.

"Utata wa hapa na pale kwa kweli umetokea lakini mimi ni mtu ambaye anapenda kuacha mambo yaliyopita yapite. Huwa sipendi sana kushikilia ugomvi. Tumetokea sana kama hatujagombana naye," Sepetu alisema.

Hamisa Mobetto kwa upande wake alifichua kwamba muigizaji huyo mkongwe amekuwa rafiki mzuri sana kwake kwa karibu muongo mmoja na akabainisha kuwa alimsaidia kukuza kazi na umaarufu wake.

"Hakuwahi kunibagua mimi. Alinifahamu hata kama sijaanza habari za usanii, alinijua kitambo tangu nilipomaliza shule," alisema.

Kwa muda mrefu, malkia hao wawili wa Bongo wamekuwa wakidaiwa kuzozana hasa kutokana na matukio yao ya nyuma. Wawili hao wamewahi kuchumbiana na staa wa Bongo Diamond Platnumz katika nyakati tofauti.

Mobetto ambaye ndiye wa mwisho kati yao kuwa kwenye mahusiano na bosi huyo wa WCB anaaminika kuwa na mvulana, Dylan Abdul Naseeb. Hata hivyo kumekuwa na mvutano kati ya wawili hao kuhusu mtoto huyo.

Mwaka jana, mwanamitindo huyo alilalamika kwamba Diamond amemtelekeza mtoto na kudai hajui sababu yake. Hii ni baada ya mzazi huyo mwenzake kutomsherehekea mtoto huyo akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

"Kusema ukweli sifahamu kwa nini nadhani hilo swali ni vizuri sana akiulizwa yeye mwenyewe binafsi mi ntakua sina majibu na mi si mtu ambaye anauliza nadhani ni maamuzi tu mtu unaamka tu asubui unaamua," alisema.

Diamond na Wema Sepetu walichumbiana kati ya mwaka wa 2012 na 2014 ila hawakuwahi kupata mtoto pamoja.

Katika mahojiano ya awali, muigizaji huyo aliwahi kumshtumu Diamond kwa kuwa mpenzi mwenye vurugu.