Kwa nini serikali inataka kusitisha kampeini za 'hustler'

Muhtasari

• Ni jambo la kusikitisha kwamba baadhi ya watu wanatumia visivyo udhaifa wa wananachi wetu kutokana na athari za kiuchumi za Covid-19.

• Watu wawili waliuawa baada ya vurugu kuzuka katika mkutano wa Ruto katika eneo la Kenol kaunti ya Murang'a siku ya Jumapili. 

• Ruto amekuwa akiwakabidhi vijana na akina mama bidhaa kama vile mikokoteni, pikipiki na bidhaa zinginezo.

 

Taarifa ya Julius Otieno

Serikali imeanzisha mikakati ya kuwekea vikwazo kampeini za 'hustler' zinazoongozwa na naibu rais William Ruto, na kumshtumu Ruto kwa kutumia masaibu ya vijana kuligawanya taifa. 

Katika taarifa iliyolenga mikutano ya naibu rais, kamati ya kitaifa ya kutoa ushauri kuhusu masuala ya usalama ilitoa onyo dhidi ya kampeini ambazo zinalenga kuchochea vijana wasiokuwa na ajira. 

“Ni jambo la kusikitisha kwamba baadhi ya watu wanatumia visivyo udhaifa wa wananachi wetu kutokana na athari za kiuchumi za Covid-19,” Mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua alisema.

 Naibu rais amekuwa akitumia kauli mbiu ya 'hustler' kuinua hisia za wafuasi wake kwa kampeini za 2022 hatua ambayo imeonekana kumlenga rais Uhuru Kenyatta na mwandani wake wa kisiasa Raila Odinga. 

Ruto amekuwa akiwakabidhi vijana na akina mama bidhaa kama vile mikokoteni, pikipiki na kuwataka kuwachana na wanasiasa wanaotoka familia za mabwenyenye ambao walikuwa uongozini.

Katika hatua ambayo imeashiria wazi kuwa rais Uhuru Kenyatta na naibu wake huenda hawali sahani moja, kamati hiyo ya usalama ili mlaumu moja kwa moja Ruto kwa uchochezi.

 “Watu hao katika jaribio la kuafikia ajenda zao za kibinafsi wanawachochea vijana ambao wanahofia maisha yao ya kesho. Wanajaribu kuwachochea vijana kuwa na misimamo mikali kiasi cha kwamba baadhi yao wamepigana na kuuana,” Kinyua alisema.

“Matamshi yasiodhibitiwa na uchochezi wa kisiasa mikutanoni vinaendelea kuhujumu sheria na utulivu nchini. Utovu huu wa sheria umepelekea makabiliano makali baina  ya makundi mbali mbali na hivyo kutishia usalama wa kitaifa.”

Kamati hiyo ilitoa onyo kali kwa wale ambao jumbe zao za kampeni zinahujumu haki za kibinafsi  hali ambayo huenda ikazua ubaguzi wa watu kwa misingi ya uwezo wao kiuchumi. 

Akitoa taarifa hiyo siku ya Jumatano, Kinyua alikuwa ameandamana na Solisita mkuu Kennedy Ogeto, Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai, naibu mkuu wa utumishi wa umma Wanyama Musiambo, katibu wa kudumu wa usalama wa ndani Karanja Kibicho na mwenzake wa mashauri ya kigeni Macharia Kamau.

Aliagiza kwamba mikutano yote bila kujali cheo cha mtu kiuchumi, kijamii na kisiasa lazima ipate idhini ya polisi siku tatu kabla ya kufanyika. 

Mkutano huo  wa kamati ya usalama ulijiri siku chache tu baada ya kinara wa ODM Raila Odinga kuitaka serikali kusitisha kampeini za mapoema za naibu rais ambazo alidai zinaligawanya taifa. 

Watu wawili waliuawa baada ya vurugu kuzuka katika mkutano wa Ruto katika eneo la Kenol kaunti ya Murang'a siku ya Jumapili. 

Hata hivyo bado haijulikani vile serikali inalenga kusitisha mikutano ya Ruto na makundi ya vijana na kinamama katika makao yake rasmi mtaani Karen. Nairobi na nyumbani kwa mashambani eneo la Sugoi kaunti ya Uasin Gishu.