MAJIBU YA ATWOLI

Tusherehekee watu maarufu wakati wangali hai! Atwoli

Amesema kuwa hisia zinazotolewa mitandaoni kuhusiana na kubadilishwa kwa jina la barabara ya Dik Dik kuwa Barabara ya Francis Atwoli zinashinikizwa na ukabila.

Muhtasari

•Tahariri iliyokuwa imeandikwa kwenye gazeti la The Star siku ya Jumatano ilipendekeza kukomeshwa kwa kubatiza mitaa na barabara nchini Kenya majina ya watu walio hai.

•Atwoli amedai kuwa nchi ya Kenya imekuwa na mashujaa waliofaa kusherehekewa wakiwa hai.

Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli
Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli

Katibu mkuu wa COTU, Francis Atwoli amewataka Wakenya kusherehekea mashujaa wangali hai.

Kupitia ujumbe wa kujibu tahariri iliyoandikwa na gazeti la The Star, Atwoli amesema kuwa tendo la kusherehekea mashujaa wangali hai linawapa motisha kuendelea kutoa huduma zao kwa kujitolea na kuendelea kufanya matendo mema ya kusaidia jamii.

Tahariri iliyokuwa imeandikwa kwenye gazeti la The Star siku ya Jumatano ilipendekeza kukomeshwa kwa kubatiza mitaa na barabara nchini Kenya majina ya watu walio hai.

Hamna shida ikiwa kaunti ya Nairobi itapatia mitaa majina ya watu walioaga. Miezi tatu iliyopita,barabara ya Accra ilibadilishwa jina na kuitwa barabara ya Kenneth Matiba. Hakuna aliyeteta. Vivyo hivyo, hitakuwa sawa kaunti ya Nairobi ikibatiza barabara baada ya  Chris Kirubi. Historia yake inajulikana na imekamilika” Tahariri hiyo ilisoma.

Atwoli alikashifu tahariri hiyo huku akisema kuwa  hakuna shida kwa kuwapa heshima wanaume na wanawake maarufu ambao nchi ya Kenya imetoa wikiwa hai bado.

Akijibu maoni hayo, Atwoli amedai kuwa nchi ya Kenya imekuwa na mashujaa waliofaa kusherehekewa wakiwa hai.

“Inasaidiaje kusherehekea Wangari Maathai, Oginga Odinga, Masinde Muliro, Tom Mboya na Ronald Ngala kwa sasa? Hawa ni watu waliofaa kusherehekewa walipokuwa hai bado. Je, hatufai kusherehekea wanariadha wakubwa kama Eliud Kipchoge sasa?” Atwoli aliandika.

Atwoli alisema kuwa wale wanaokashifu serikali kwa kusherehekea wanaume na wanawake maarufu wakiwa bado hai ndio bado wanasuta serikali vikali wakati inaibuka kuwa haiwatunzi watu walioleta heshima nchini.

Mfano ni wakati iliibuka kuwa Conjestina Achieng, mwanandondi  aliyeletea nchi ya Kenya heshima alikuwa ametelekezwa. Wakenya wengi walisuta serikali  kwenye mitandao ya kijamii  kwa kumtelekeza badala ya kumtumikia kama mwanariadha mkubwa. Nashangaa nini ingefanyika ikiwa serikali iliamua kuita ulingo wa ndondi ama nyanja kuu baada ya jina lake. Kwani hajahitimu? " Atwoli  aliendelea kusema.

Alitaja kuwa hayati Jomo Kenyatta na Moi  na rais mstaafu Mwai Kibaki walipewa heshima na kusherekewa wakiwa hai, jambo ambalo alisema ni nzuri.

Atwoli amewataka Wakenya kusitisha tabia ya kuatibu vitu kwa ajili tu.

Amesema kuwa hisia zinazotolewa mitandaoni kuhusiana na  kubadilishwa kwa jina la barabara ya Dik Dik kuwa Barabara ya Francis Atwoli zinashinikizwa na ukabila.