Raia wa kigeni 104 wanaotuhumiwa kuwa wahasiriwa wa ulanguzi wa binadamu wakamatwa Juja

104 hao walikuwa wamefungiwa ndani ya nyumba moja katika kijiji cha Thome, Juja.

Muhtasari

•Kamanda wa polisi maeneo hayo, Dorothy Migarusha alisema kuwa polisi walishambulia nyumba hiyo Jumatatu asubuhi baada ya mkazi wa maeneo hayo kuwajulishwa kuhusu jambo tatanishi lililokuwa linaendelea pale.

•Migarusha alisema kuwa wageni hao ambao wana umri wa miaka kati ya miaka 15-40 hawakuwa na vitambulisho.

Baadhi ya raia wa kigemi ambao walipatikana Juja
Baadhi ya raia wa kigemi ambao walipatikana Juja
Image: JOHN KAMAU

Polisi maeneo ya Juja wamekamata raia wa kigeni 104 ambao wanatuhumiwa kuwa wahasiriwa wa ulanguzi wa binadamu.

104 hao ambao wanadhaniwa kuwa raia wa Ethiopia walikuwa wamefungiwa ndani  ya nyumba moja katika kijiji cha Thome, Juja.

Kamanda wa polisi maeneo hayo, Dorothy Migarusha alisema kuwa polisi walishambulia nyumba hiyo Jumatatu asubuhi baada ya mkazi wa maeneo hayo kuwajulishwa kuhusu jambo tatanishi lililokuwa linaendelea pale.

"Maafisa wetu walipatiwa habari na baadhi ya wakazi ambao walishuku kuwa kuna biashara haramu ilikuwa inaendelea kwa nyumba hiyo. Walisema kuwa wangeona magari yakiingia na kutoka pale mida ya usiku. Tulishambulia nyumba hiyo na kuwapata raia hao wa kigeni" Migarusha alisema.

Migarusha alisema kuwa wageni hao ambao wana umri wa miaka kati ya miaka 15-40 hawakuwa na vitambulisho.

Upelelezi kubaini kina nani walikuwa wanaendeleza biashara hiyo umeanza.

Baadhi ya raia wa kigeni ambao walipatikana Juja
Baadhi ya raia wa kigeni ambao walipatikana Juja
Image: JOHN KAMAU

Watu wawili ambao wamekuwa wakiwapikia wageni hao walitiwa mbaroni na watasaidia kwenye upelelezi.

Majirani waliarifu wanahabari kuwa walianza kuwa na shuku baada ya kuwaona raia wa kigeni 6  wakijaribu kupanda ukuta wa nyumba walimokuwa wamefungiwa ili kutoroka.

Majirani hao ambao walidhani kuwa ni wezi waliwakimbiza sita hao na kuwarejesha pale kwa nyumba ile. Hapo ndipo wakagundua kuwa walikuwa wengi ndani ya nyumba hiyo.

"Tulijulisha polisi kwani tulishuku kuwa walikuwa wanapanga kutekeleza uhalifu maeneo haya" Lawrence Kahoro alisema.

Inadaiwa kuwa walikuwa wamekaa pale ndani kwa takriban wiki mbili.