(+Picha) Fahamu mbunge wa Kenya anayetumia walinzi wa kike

Jambo lingine ambalo lilivutia watu ni kwamba wasichana wanaomlinda Anab walikuwa wamejistiri kwa hijab na walikuwa na silaha.

Muhtasari

•Anab Subow Gure, mbunge wa Garissa, alivutia mitandao ya kijamii na vyombo ya habari vya Kenya baada ya walinzi wake wa kike kuonekana

Image: ANAB SUBOW GURE

Watu wengi wanakumbuka kwamba walinzi wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi walikuwa wasichana, lakini sasa hii imefanywa tena na mwanamke Msomali katika bunge la Kenya.

Anab Subow Gure, mbunge wa Garissa, alivutia mitandao ya kijamii na vyombo ya habari vya Kenya baada ya walinzi wake wa kike kuonekana.

Jambo lingine ambalo lilivutia watu ni kwamba wasichana wanaomlinda Anab walikuwa wamejistiri kwa hijab na walikuwa na silaha.

Wasichana wawili ambao wanasemekana kuwa walinzi wake pia hubeba risasi na silaha.

Anab Subow Gure wakati mmoja alichapisha picha ya Rais Mohamed Abdullahi Farmajo na bendera ya Somalia, na kusababisha madai mengi kwamba nchi nyingine inamuunga mkono.

Lakini alikanusha madai yote, akisema picha hiyo ilikuwa ya kufunguliwa kwa ubalozi wa Somalia jijini Nairobi.

Anab, mtetezi wa wazi wa haki za watu anaowawakilisha, aliliambia gazeti la Nation katika mahojiano: "Nimechagua wanawake katika vikosi vya usalama. Ninaamini wasichana wanaweza kufanya vizuri zaidi kuliko wanaume."

Picha za kuvutia zilipigwa wakati wa ziara ya eneo lenye hatari kubwa.

Akielezea hili, alisema: "Safari yangu ilikuwa ya umbali wa kilometa 10 kutoka mpaka wa Somalia na nilihitaji gari moja la usalama ili kuongozana nami. Mahali nilipokwenda nilishambuliwa hivi karibuni na kikundi cha al-Shabaab, kwa hivyo sitaki kuhatarisha maisha yangu. "

Lakini anasema hii si mara ya kwanza kuwa na walinzi wanawake.

''Hapana, ninasafiri usawa wa mpaka ule, mara zote ni mimi na walinzi wangu wa kike,'' alisema.

Wakati wa ziara yake huko alifanya mikutano na wakazi kujadili usalama na maisha, kwani ni sehemu ya Mkoa wa Garissa.

Je! Ni faida gani maalum za walinzi wa kike?

Mbunge Anab Subow Gure alielezea ni kwanini anapendelea wanawake , anasema kuna faida ya ziada.

"Kuna vitu vya binafsi vya wanawake ambavyo wakati mwingine nasahau kubeba, kwa hivyo ninaweza kupata kwenye mifuko ya walinzi wangu wa kike . Pia kuna taarifa ambazo siwezi kusema kwa walinzi wa kiume."

Alipoulizwa jinsi alivyoanza na walinzi wanawake alisema hataki kutoa maelezo zaidi juu ya wanawake, kwani ni habari yao wenyewe.

Ni mara ya kwanza kwa mbunge Anab kuonekana na mlinzi wa kike wa Somalia.

Watu wengine wametoa hoja wakipendekeza kwamba wanasiasa wote wanawake wawe na walinzi wa kike.