Mwanamume amuua mwanawe na kisha kujitia kitanzi

Muhtasari

• Kulingana na taarifa ambazo zilichapishwa na wakurugenzi wakuu wa upelelezi DCI, familia yam toto huyo inayoishi katika mtaa wa Embakasi jijini Nairobi inalilia haki ya mwanao Derick Okeyo, 3

• Inasemekana Derrick alitekwa nyara na babake wa damu na kisha kuuawa katika kisa ambacho kimewaacha wakaazi wengi mtaani humo vinywa wazi.

Embakasi, Nairobi
Embakasi, Nairobi
Image: HISANI

Mwanaume mmoja mtaani Embakasi amemuuwa mwanawe wa kiume na kisha kujitia kitanzi katika kile kinatajwa kuwa mzozo wa kimapenzi.

Kulingana na taarifa ambazo zilichapishwa na idara ya ya DCI, familia ya mtoto huyo inayoishi katika mtaa wa Embakasi jijini Nairobi inalilia haki ya mwanao Derick Okeyo, 3, aliyetekwa nyara na babake mzazi na kisha kuuawa katika kisa ambacho kimewaacha wakaazi wengi vinywa wazi.

Kulingana na mamake mtoto huyo kwa jina Nancy Adhiambo,  walikuwa washatengana na mumewe wa kwanza, Victor Ayieko, 30, ambaye ni babake mtoto na kuolewa na mwanamume wa pili ambaye walikuwa wanaishi naye kabla ya mume wa kwanza kuvizia na kutoweka na mtoto Derrick ambaye baadae alimuuwa na kujinyonga pia.

DCI imesema muuaji  alinyata na kuponyoka na mtoto kabla ya kumtendea unyama huo.

Mamake mtoto Derrick alikuwa ameenda katika mishemishe za siku na mumewe wa pili Chistopher Okeyo ila baada ya kurudi wakapata mtoto wao hayupo.

Inaarifiwa wapenzi hao walijaribu kumtafuta mwanao ila juhudi zote ziligonga mwamba na hapo ndipo walipodokezewa na majirani kwamba kuna mwanamume aliyevizia na kutoroka na mwanawe.

Majirani walitoa maelezo ya muonekano wa mwanamume huyo na hapo Nancy akajua moja kwa moja maelezo hayo yanamfaa mumewe wa awali ambaye maelezo zaidi yalionyesha aliondoka akitumia pikipiki pamoja na mwanao Derrick.

crime scene 1
crime scene 1
Image: HISANI

Baada ya maelezo hayo, waliondoka kwa upesi hadi kwa nyumba ya mumewe wa awali katika mtaa wa mabanda wa Mukuru kwa Njenga na kupata mlango umefungwa jambo lililowapelekea kujaribu kuvunja mlango huo na walichokiona mule ndani kikawa ni cha kusikitisha mno.

Walipigwa na butwaa baada ya kukaribishwa na kimya kikuu cha picha ya maiti ya mwanao Derrick ikiwa imelazwa kitandani mwa babake huku mwili wa mwanaume huyo ukiwa umening’inia kwenye paa la ndani pembezoni mwa nyaya ya umeme mithili ya popo

Maelezo ya kujiua kwake yalipatikana katika kijikaratasi pamoja na noti ya shilingi mia tano. Katika maelezo hayo, marehemu alitoa maelezo kwa mkewe wa zamani kutumia mia tano hiyo kununua mjazo wa simu wenye thamani ya kiwango sawa na kuwapa taarifa ndugu, jamaa na marafiki kuhusu vifo vya wawili hao.

DCI imewataka wazazi kuwa makini na mazingira wanayowaacha Watoto wao, kutokana na visa vingi vya watoto kupotea haswa jijini Nairobi.