Nelson Havi: Nitapambana na rais Kenyatta kortini katika kesi ya ardhi ya chuo cha KU

Nelson Havi alisema chuo cha KU kilimtafuta kutaka awe wakili wao

Muhtasari

• Kesi hiyo itatajwa na kusikilizwa tarehe 26.7.2022

Rais Uhuru Kenyatta na wakili Nelson Havi
Rais Uhuru Kenyatta na wakili Nelson Havi
Image: Facebook///State House Kenya, Nelson Havi

Mwaniaji ubunge Westlands jijini Nairobi Nelson Havi anasema uongozi wa chuo kikuu cha Kenyatta ukiongozwa na naibu chansela, wafanyakazi wa ofisini na viongozi wa wanafunzi walimtafuta ili kuwasimamia kama wakili katika kesi ya kupinga hatua ya rais Uhuru Kenyatta kunyakua sehemu ya ardhi ya chuo hicho ili kujenga kuto cha shirika la afya duniani WHO.

Havi alipakia makaratasi kadhaa ya kesi hiyo kwenye ukurasa wake wa Facebook na kusema kwamba baada ya tathmini ya muda mrefu, hatimaye alikubali kuwakilisha chuo cha Kenyatta katika kesi hiyo ambayo alifichua inasikilizwa mnamo tarehe 26 mwezi huu, wiki kesho.

Mzozo baina ya uongozi wa chuo cha Kenyatta na rais Uhuru Kenyatta ulianza wiki mbili zilizopita pale ambapo rais Kenyatta alimzomea hadharani naibu chansela wa chuo hicho Paul Wainaina kuhusu kile alisema kwamba profesa huyo wa chuo anajaribu kukataa ardhi kutumika kwa miradi ya serikali hali ya kuwa chuo chenyewe ni cha serikali pia.

Rais Kenyatta alizidi kutoa tahadhari kwa watu wote wenye kupinga miradi yake na kusema kwamba alikuwa na wiki tatu ofisini kama rais na angefanya kila awezalo ili kuhakikisha kwamba wote wanaompinga wataenda na yeye nyumbani.

Siku chache baadae palizuka uvumi mitandaoni kwamba naibu chansela profesa Paul Wainaina amejiuzulu baada ya shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi serikalini, madai ambayo hayakudhibitishwa mpaka sasa.

Uongozi wa chuo hicho ulipinga vikali sehemu ya ardhi yake kuchukuliwa na serikali kwa mradi wa WHO huku wakisema kwamba walikuwa na mipango mingine na ardhi hiyo ambayo rais Kenyatta alikuwa anataka kunyakua ili kuwezesha mradi huo kujengwa.