Kijana wa miaka 17 amuua babake kwa kumgonga kichwani kufuatia mzozo, Nandi

Hasira zilimpanda kijana huyo na akachukua chuma kizito ambacho alitumia kumgonga babake kichwani hadi akapoteza fahamu.

Muhtasari

•Wawili hao wanaripotiwa kuzozana usiku wa Jumatatu  kuhusu suala ambalo halijabainika kufikia sasa.

•Majirani walimkimbiza mzee huyo katika hospitali ya Miteitei ambako alifariki alipokuwa anapokea matibabu.

crime scene 1
crime scene 1

Mwanaume wa miaka 42 kutoka maeneo ya Kapkoros kaunti ya Nandi  aliangamia kutokana na majeraha mabaya baada kuhusika kwenye vita na mwanawe wa miaka 17.

Wawili hao wanaripotiwa kuzozana usiku wa Jumatatu  kuhusu suala ambalo halijabainika kufikia sasa.

Kulingana na DCI, hasira zilimpanda kijana huyo na akachukua chuma  kizito ambacho alitumia kumgonga babake kichwani hadi akapoteza fahamu.

Majirani walimkimbiza mzee huyo katika hospitali ya Miteitei ambako alifariki alipokuwa anapokea matibabu.

Kijana huyo alikamatwa na anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nandi akisubiri kusomewa mashtaka dhidi yake.

Kwingineko polisi upande wa Kiamunyeki kaunti ya Nakuru wanamsaka jamaa mmoja anayedaiwa kuua mke wake kwa kumdunga shingoni kwa kutumia kisu huku bintiye wa miaka 10 akitazama.

John Mburu Njuguna, anaripotiwa kumgombeza mkewe  wa miaka 34 wakiwa kwenye lango nyumbani kwao kabla yake kuchukua kisu na kumdunga shingoni usiku wa Jumatano.

Binti yao wa miaka 10 ambaye alishuhudia yote aliangua kilio kikubwa ambacho kiliita majirani waliofanya juhudi kujaribu kumwokoa mwanamke huyo ila akakata roho.

Kuona umati mkubwa wa watu wenye ghadhabu ukiwa umejumuika mshukiwa alitimuka mbio na kutoweka asijulikane aliko hadi kufikia sasa.