•Alipokuwa anathibitisha tukio hilo, naibu chifu wa eneo hilo Bw Duncan Oketch alisema kuwa marehemu aliaga baada ya kugusa waya wa umeme ambao ulikuwa unasambaza stima kiharamu kwa nyumba zilizo karibu na shamba lake.
Habari na Faith Matete
Hali ya majonzi imetanda katika kijiji cha Arunda kaunti ya Homabay baada ya mwanamke mmoja kuuawa na nguvu za umeme akiwa shambani kwake.
Jane Opala 59, alikuwa anapanda mahindi kwenye shamba lake wakati msiba huo ulitokea.
Opala alishika waya wa umeme akijaribu kuuondoa kwa njia ili aweze kupanda bila kufahamu ulikuwa na stima na akafariki papo hapo.
Alipokuwa anathibitisha tukio hilo, naibu chifu wa eneo hilo Bw Duncan Oketch alisema kuwa marehemu aliaga baada ya kugusa waya wa umeme ambao ulikuwa unasambaza stima kiharamu kwa nyumba zilizo karibu na shamba lake.
Bw Oketch aliita Kenya Power kufanya msako katika eneo hilo ili kuwanasa wale ambao wameweka stima kwa manyumba zao kiharamu.
Raia walionywa dhidi ya kujihusisha na tabia hiyo kwani inasababisha maafa na ni ukiukaji wa sheria ambapo mtu anaweza kukamatwa na kushtakiwa.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya Homabay huku polisi wakianza msako wa kuwinda ambao wanasambaza nguvu za umeme kiharamu.